27 February 2013

Mgogoro wa Kagasheki, Meya bado washika kasi



Theonestina Juma na Livinus Feruzi, Bukoba

MGOGORO wa kisiasa uliopo kati ya Meya wa Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Dkt. Anatory Amani na Mbunge wa
jimbo hilo, Balozi Khamis Kagasheki, umeanza kuathiri
vikao vya Baraza la Madini wa Manispaa hiyo.

Hali hiyo inatokana na idadi ndogo ya madiwani waliohudhuria kikao cha kujadili bajeti ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kutokana na mgogoro huo.

Mkutano huo ulikuwa uanze saa nne asubuhi lakini ulishindwa kufanyika kwa mujibu wa kanuni kutokana na idadi ndogo ya madiwani waliofika ukumbini hapo.

Hata hivyo, baada ya wajumbe wa mkutano huo kusubiriwa kwa muda mrefuhadi ilipofika saa 5:45, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Khamis Kaputa, aliwaomba makatibu wa madiwani kutoka vyama vinavyoongoza halmashauri hiyo, wakutane ofisini kwake.

Baada ya muda mfupi, wajumbe wa mkutano huo waliambiwa mkutano huo unahairishwa kwa muda badala yake utaanza saa
sita lakini baada ya muda huo, Bw. Kaputa alisema idadi ya madiwani waliopaswa kushiriki mkutano huo haijatimia.

“Halmashauri ina madiwani 24 hivyo nusu yao kwa maana ya madiwani 12, kama wangekuwepo mkutano huo ungeendelea
lakini waliohudhuria ni 11.

“Bajeti ndio uhai wa wananchi...naomba Meya uhairishe mkutano
na sisi tutaijulisha Serikali sababu za kukwama kwa bajeti hii ili watupe maelekezo,” alisema Bw. Kaputa.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Zimpora Pangani, alisema kitendo cha baadhi ya madiwani kukwamisha maendeleo ya wananchi kwa sababu za mgogoro wa kisiasa ambao unaendelea kupatiwa
ufumbuzi ni kutowatendea haki wananchi waliowachagua.

Alisema viongozi wa Serikali na CCM wanafanyia kazi malalamiko ya baadhi ya madiwani ndio maana hata Makamu Mwenyekiti wa chama Taifa, Bw. Philip Mangula, alikwenda kusikiliza malalamiko
ya wadiwani.

Aliongeza kuwa, wakati mgogoro huo ukiendelea kupatiwa ufumbuzi, Serikali iliona si vizuri maendeleo ya wananchi
kukwama na kuwataka watendaji wa halmashauri chini ya Mkurungenzi, kuendelea na kazi kwa mujibu wa mikataba
yao bila kujiingiza katika masuala ya kisiasa.

Akitangaza kuahirisha kwa baraza hilo, Dkt. Amani alisema
kitendo cha baraza hilo kutojadili na kupitisha bajeti ya
maendeleo ni kutowatendea haki wananchi.

“Bajeti ni kwa ajili ya wananchi...zaidi ya asilimia 90 ni fedha zinazotolewa na Serikali Kuu pamoja na wahisani hivyo kitendo
hicho ni sawa na kuieleza Serikali Bukoba hawahitaji fedha hizo,” alisema Dkt. Amani.


Hivi karibuni, kumeibuka mgogogo ambao unamuhusisha Dkt. Amani pamoja na Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye anapinga utekelezaji wa baadhi ya
miradi akidai haiko wazi wakati Meya akidai miradi hiyo imepitishwa na vikao halali vya halmashauri.

Baadhi ya miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa soko jipya la kisasa, jengo la kitega uchumi lenye ghorofa 10, Kituo Kikuu cha Mabasi pamoja na upimaji viwanja 5,000.

Inadaiwa kuwa, madiwani waliohudhuria kikao hicho ni wale wanaomuunga mkono Dkt. Amani


No comments:

Post a Comment