11 February 2013

Viongozi wekeni kando itikadi zenu-CCM



 
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) wilayani Meatu mkoani Simiyu kimewataka wanasiasa wote wilayani humo kuweka pembeni tofauti za vyama vyao vya siasa na kushughulikia kwa pamoja tatizo la kushuka kwa kiwango cha elimu kwa watoto mashuleni.

 
Wito huo umetolewa wiki iliyopita na mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Meatu, Juma Mwiburi alipokuwa akitoa mchango wake katika kikao cha Kongamano la wadau wa elimu wilayani humo lililofanyika kwa ajili ya kutafuta njia muafaka ya kuboresha elimu
kwa watoto wa shule za msingi na sekondari.
 
Mwibura alisema ili kukabiliana na tatizo la kushuka kwa kiwango cha elimu katika
wilaya hiyo ambayo kwa miaka mitano imekuwa ikishika nafasi ya mwisho kitaifa kwenye
matokeo ya mitihani ya kumaliza darasa la saba, ni vyema kila mkazi wa wilaya hiyo akashiriki kikamilifu katika mkakati huo wa kuboresha elimu.
 
“Katika mapambano haya ya kuitoa wilaya yetu katika dimbwi la ujinga ni muhimu kila mwana Meatu sasa ajitoe kwa moyo mmoja na wa dhati kushiriki katika kushughulikia changamoto za elimu zilizopo katika wilaya yetu zinazosababisha watoto wetu kukosa
elimu waliyoitarajia,”
 
“Ni aibu kwa wilaya yetu kuendelea kuburuza mkia kila mwaka katika matokeo ya kitaifa ya kumaliza darasa la saba na hata matokeo ya kumaliza kidato cha nne ni hivyo hivyo na ni aibu kuyataja hapa, sasa kila mmoja wetu awe ni askari katika vita
hii, tuweke pembeni tofauti za vyama vyetu vya kisiasa na tushikamane sote,” alisema
Mwiburi.
 
Awali akifungua kongamano hilo , mkuu wa wilaya ya Meatu, Rosemary Kirigini alisema wilaya ya Meatu inakabiliwa na tatizo kubwa la kushuka kwa kiwango cha elimu katika shule za msingi na sekondari hali ambayo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na changamoto
zinazoikabili sekta ya elimu.
 
Kirigini alisema baadhi ya changamoto ni pamoja na umbali wa shule, mimba kwa watoto wa kike, ukosefu wa miundo mbinu muhimu, ikiwemo hosteli, viti na madawati na pia baadhi ya wazazi kugoma kuwaruhusu watoto wao wa kike kuishi katika hosteli
zilizokwishajengwa.
 
“Pamoja na kwamba kuna shule ambazo hivi saa zina hosteli, lakini wapo wazazi wanaogoma kuruhusu watoto wao kuishi katika hosteli hizo na badala yake wanawapangia vyumba mitaani, hali hii tumeikuta huko katika sekondari za Nyalanja na Bukundi, zina hosteli lakini hakuna watoto wanaoishi humo,”
 
“Hali ya kuishi maisha ya kupanga mitaani imesababisha watoto wengi wa kike washindwe kumaliza masomo yao kutokana na kupewa mimba na wengine tumekuta wameisha olewa, sasa kupitia kongamano hili tushirikiane kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo , wazazi watueleze ni kwa nini hawapendi watoto waishi hosteli,” alieleza Kirigini.
 
Alisema changamoto nyingi iliyobainika ni walimu kutotimiza wajibu wao kikamilifu huku kila siku wakihangaika kudai haki na kwamba wengi wanadai haki hizo bila ya kutimiza wajibu na baadhi wamediriki kutoroka katika vituo vya kazi na kufanya
biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia pikipiki za bodaboda.
 
Mkuu huyo alisema baada ya uongozi wa serikali kubaini tatizo la kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani humo yenye shule za msingi 111 na wanafunzi wapatao 62,930 kiasi cha kuwa na kiwango cha ufaulu wa asilimia 27.6 umeona ni muhimu kufanyika kwa kongamano hilo ili kutafuta mbinu za kukabiliana na hali hiyo.

No comments:

Post a Comment