11 February 2013
Milioni 60/= upotea kila mwaka-TANESCO
Na Mariam Mziwanda
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Temeke limeendelea na kampeni ya ukamataji wa wezi wa umeme katika mkoa huo ili kuongeza mapato ya shirika ambayo zaidi ya milioni 60 zinapotea kila mwezi mkoani humo.
Akizungumza Dar es salaam juzi katika Oparesheni ya KWEU inayoendelea Kaimu Meneja wa Mkoa huo ambaye pia ni Mhandisi Muandamizi Bw.Stephan Mfundo alisema kuwa Temeke ni kitovu cha wizi wa umeme, ambapo wateja wake asilimia kubwa ndio chanzo cha upotevu wa mapato.
"Wizi wa umeme Temeke ni tatizo kubwa na zaidi ya milioni 60 kwa mwezi zinapotea hivyo shirika hilo linajitahidi kubuni mbinu mpya ili kubaini wezi wa shirika na wahalifu wa miundombinu, ambao wanachangia kushuka kwa maendeleo nchini wezi hawa ni watu hatari hawahitaji kuchekewa hivyo wilaya tumeadhimia kuwadhibiti ipasavyo,"alisema
Alieleza kuwa mikakati iliyopo ni kuhakikisha wanaongeza timu ya wakaguzi waadilifu na waaminifu ili kufikia malengo katika wilaya hiyo.
Katika Oparesheni hiyo TANESCO imefanikiwa kukata umeme kwa baadhi ya wateja wake ikiwemo hoteli ya Leopard Inn kutokana na kubaini matumizi ya umeme hewa na uchezaji wa mita uliopelekea mteja huyo kulipa asilimia ndogo inayopita katika mita yake na ubadilishaji wa siri za mita.
Naye Mdhibiti wa Mapato na Mkaguzi kutoka Wizara ya Nishati na Madini Bw.Cristian Saimon alieleza kuhangazwa na mbinu wanazotumia mkoa wa Temeke ambazo kwa asilimia kubwa zinafanana hasa kwa wateja wakubwa na wafanyabiashara hivyo kuwa na mashaka ya kuhusika kwa vishoka aina moja na kutangaza msako mkali.
Shirika hilo lilieleza kuwa mbali na hatua hizo za awali za ukataji wa umeme pia wateja waliohusika watafanyiwa tathimini ya malipo ya umeme waliotumia na faini na baada ya kuomba tena huduma watafungiwa mita mpya zinazopita moja kwa moja katika nguzo ili kupunguza uharifu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment