11 February 2013

'Wananchi wekeni jitihada katika masomo ya sayansi'



Na Neema Malley

WANANCHI wametakiwa kutambua kuwa maendeleo ya  nchi hayawezi kuja bila sayansi hivyo wanatakiwa kuweka jitihada kubwa katika masomo ya sayansi.


Hayo yalisemwa hivi karibuni Jijini Dar es Salaam na rais wa taaluma ya sayansi Tanzania (TAAS) Esther Mwaikumbo alipokuwa kwenye sherehe ya kuwasimika wataalamu 60  wa masuala ya sayansi walioingia kwenye chama cha TAAS.

Alisema kuwa kwa sasa chama chao kinataka kujikita kwa wanafunzi mashuleni ili wanafunzi wapende kusoma masomo ya sayansi na kupata wanasayansi wengi nchini ili nchi iweze kuendelea kupitia wanasayansi.

Aidha rais huyo alisema kuwa moja ya changamoto zinazowakabili katika sekta ya sayansi ni vijana wengi hawasomi masomo ya sayansi kwa kisingizio cha masomo hayo kuwa magumu.

Alisema kuwa ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo la watu kutokupenda kusoma masomo ya sayansi taasisi hiyo imejipanga kuanzisha kamusi ya maneno ya sayansi ambayo itasaidia maneno ya sayansi kueleweka kwa wanafunzi.

Alisema kuwa kutokana na idadi ndogo ya watafiti waliojiunga katika taasisi hiyo ya wasuala ya kisayansi inaonyesha kuwa watu wengi hawasomi masomo ya sayansi hivyo kufanya nchi kutoendelea kwa haraka.

"Hakuna nchi isiyoendelea bila kuwa na wanasayansi wanafunzi wengi hawasomi masomo ya sayansi hivyo inachukua muda mrefu kupata maendeleo bila kuwa wa wanasayansi wa kutosha,"alisema Mwaikambo.

Hadi sasa chama hicho cha wataalamu wa utafiti wa masuala ya kisayansi kinawanachama 133, ambapo idadi hiyo inaweza kusaidia sayansi kujulikana na kufanyika kwa ufanisi mkubwa kutokana na tafiti mbalimbali watakazofanya.

No comments:

Post a Comment