11 February 2013

Mbunge anayetaka kujiuzulu ajipime mwenyewe-Mhagama


Grace Ndossa na
Mariam Mziwanda

MWENYEKITI wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho Bi.Jenista Mhagama amesema kuwa bunge halina mamlaka ya kumwamrisha Mbunge kujiudhulu bali linamtaka  yeyote anayeahidi kujiuzulu ajipime mwenyewe.

Bi. Mhagama alisema hayo mjini Dodoma jana kufuatia mapendekezo ya Mbunge wa Nzega Mkoani Tabora, Dkt. Hamis Kigwangala (CCM), alilitaka bunge limwajibishe Mbunge wa kuteuliwa  wa chama cha NCCR Mageuzi Bw. James Mbatia kutokana na kauli yake ya kulidanganya bunge.

"Wabunge naomba muelewe kuwa spika wa bunge aliunda kamati na kuipa kazi ambapo matokeo yake yaliwasilishwa hapa Bungeni juu ya mahitaji ya mbunge huyo kumtaka waziri wa elimu kuwasilisha mitaala ya elimu iliyopo na mjadala huo ulifungwa hivyo bunge hilo halina mamlaka ya kumwajibisha bali ajipime mwenyewe kutokana na ahadi yake.

Dkt. Kigwangala aliwasilisha mapendekezo yaliyosema kuwa Bw. Mbatia alilidanganya Bunge na kuvunja taratibu kwa kusema uongo na kwakua imethibitika kuwa wizara ya elimu ina mitaala ni vyema mbunge huyo kujiuzulu au kuwajibishwa na bunge.

"Kanuni ya bunge ya 63 inaeleza kuwa iwapo kiongozi yoyote atathibitika amesema uongo anatakiwa kuadhibiwa na ikiwa ni mara ya kwanza anatakiwa asihudhurie vikao vya bunge 10 na ikiwa ni mara ya pili asihudhurie bunge vikao 20 na kuomba radhi hivyo ni vyema Mbunge huyo akawajibika,"alisema Dkt. Kingwangwala.

Kwa upande wake Mbunge wa Kasulu Mjini(NCCR)Bw. Moses Machari,alisema kuwa Bw. Mbatia hajadanganya Bunge  kwani mitaala iliyowasilishwa na  Waziri wa elimu Bungeni ni pamoja na mitaala miwili inayotumika ikiwa ni ya mwaka 2005.

Alieleza kuwa kufuatia hali hiyo kilichowasilishwa bungeni  hakina ukweli bali ni uchakachuaji  na hawana imani na mitaala hiyo hivyo Mkurugenzi Mkuu wa elimu anatakiwa kuadhibiwa kwani waziri alipotakiwa kuwasilisha  alisita  hali ambayo ilitoa picha ya usanii wa mitaala hiyo.




No comments:

Post a Comment