05 February 2013

MBOWE AISHUKIA SERIKALI


Na Queen Lema, Arusha

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, ameitaka Serikali kutangaza uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata sita zilizopo jijini Arusha.


Alisema kama Serikali itashindwa kufanya hivyo bila kuchelewa, chama hicho kupitia mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless
Lema, watafanya maandamano makubwa kudai haki hiyo.

Bw. Mbowe aliyasema hayo mjini Arusha jana wakati akizungumza na wanachama pamoja na viongozi wa chama hicho katika hafla ya kukabidhiwa kiwanja cha ekari tatu ambacho kitatumika kwa ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto mkoani humo.

Alisema kitendo cha Serikali kusuasua kutangaza uchaguzi huo kinatokana na hofu ya wagombea wake kushindwa ambapo hali
hiyo inasababisha wananchi wakose uwakilishi wa kuwasemea
na kutetea haki zao katika Baraza la Madiwani.

“Serikali ikishindwa kuitisha uchaguzi ndani ya siku chache zijazo, tutalazimika kuingia barabarani kufanya maandamano makubwa pamoja na kutangaza siku ya uchaguzi,” alisema.


Katika hatua nyingine, Bw. Mbowe alisema watu wanaooona Bw. Lema hafanyi kazi za wananchi badala yake anahusika na vurugu pamoja na maandamano barabarani, wanapaswa kujua moto alionao mbunge huyo ndio unaoichanganya Serikali hasa mkoani humo.

“Mtu mwenye moto wa maendeleo huwa nampenda sana hasa
Bw. Lema ambaye amepambana leo hii tunapata eneo la kujenga hospitali, kama sio fujo zake eneo hili lisingepatikana,” alisema.

Awali akilizungumzia eneo walilopewa na Kampuni ya Mawala jijini humo, Bw. Lema alisema kampuni hiyo imetoa eneo lenye ekari tatu lenye thamani ya zaidi ya milioni 400 kwa ajili ya
ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto.

Alisema kukamilika kwa hospitali hiyo, kutaokoa maisha ya wanawake na watoto wanaokufa kutokana na kukosa huduma
nzuri za matibabu hivyo kuongeza idadi ya yatima.

“CHADEMA mkoani Arusha itahakikisha ujenzi wa hospitali hii unaanza hivi karibuni na itakuwa na huduma muhimu kwa wanawake na watoto,” alisema Bw. Lema.

No comments:

Post a Comment