05 February 2013

DC aagiza Bwana Afya akamatwe

Na Mashaka Mhando, Lushoto

MKUU wa Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, Alhaj Majid Hemed Mwanga, amemuweka ndani Bwana Afya wa Kata ya Lushoto, Bw. Emil Mtungakoa, anayedaiwa kutokuwepo ofisini kwake wiki mbili zilizopita bila kutoa taarifa zozote.


Tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki baada ya kumalizika operesheni ya usafi wa mazingira ambayo hufanyika kila Jumamosi ya kwanza ya mwezi wilayani humo.

Operesheni hiyo, ilikwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo Alhaj Mwanga alisisitiza operesheni hiyo ni ya kudumu.

Akiwa katika eneo la operesheni, Alhaj Mwanga alimuita Ofisa Afya wa Wilaya Bw. Herbert Kivunga na Bw. Mtungakoa ambaye baada ya kufika eneo hilo, alishangaa kumuona na kudai wiki
mbili zilizopita, hakuonekana ofisini bila kutoa taarifa kwa
Ofisi ya halmashauri.

“OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya), mchukue ukamuweke ndani, haiwezekani mtumishi usionekane katika eneo la kazi wiki mbili
bila kutoa taarifa...hatuwezi kuvumilia nendeni naye kituo atueleze alikuwa wapi muda wote,” alisema Alhaj Mwanga huku wananchi wakishangilia.

Alhaj Mwanga alisisitiza suala la usafi kwa kila mkazi wa Wilaya hiyo na kuuangiza Uongozi wa Umoja wa Vijana wa UVCCM, waendeleze utamaduni huo badala ya kusubiri sherehe za chama
na kuangalia uwezekano wa kusambaza mapipa ya taka ambayo yatakuwa na nembo yao.

Aliuagiza uongozi wa halmashauri, kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha wanaondoa msongamano uliopo katika Kituo Kikuu cha Mabasi mjini humo ambapo hadi Februari 9 mwaka huu, anataka kuona mpango huo uwe umeanza kutekelezwa.

Awali wakisoma risala kwa Alhaj Mwanga, Mwenyekiti wa UVCCM wilayani hapa, Bw. Antepas Mbughuni, alisema umoja
huo upo naye bega kwa bega katika kuwashughulikia watendaji
wanaoshindwa kusimamia na kutekeleza ilani ya CCM na
wanaochafua mazingira kuchukuliwa hatua.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, endelea kuwaweka ndani watendaji walioshindwa kutekeleza ilani ya chama chetu, sisi tutaendelea kukuunga mkono,” alisema Bw. Mbughuni.

No comments:

Post a Comment