26 February 2013

Maiti sita zapatikana katika Ziwa Victoria



Na Jovither Kaijage, Ukerewe

MIILI ya watu  watano waliopoteza maisha kwenye ajali ya kuzama kwa mitumbwi miwili katika Ziwa Victoria, Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza hivi Karibuni, imepatikana.


Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Mery Tesha, amesema kupatikana kwa miili hiyo, kunafanya idadi ya watu waliopoteza maisha katika
ajali hizo kufikia sita hadi jana asubuhi.

Alisema kutokana na ajali hizo, uongozi wa Wilaya hiyo umetoa
lita 100 za mafuta  ya petroli ili kusaidi kazi ya kutafuta miili ya
watu wengine ambao wanahofiwa kupoteza maisha.

Akithibitisha kupokea msaada huo, Katibu Tarafa ya Ilangala, Bw.  Joseph Maiga, alisema tayari wametuma mitumbwi mitano katika eneo la tukio ili kusaidia shughuri hiyo.

Waliopoteza maisha katika mtumbwi wa abiria unaoitwa Mv. Yeova wenye namba  TMZ 010366, ambao ulipigwa na radi juzi usiku ni Jumanne Msila (37) na Vedastus Kumi (40), wote wakazi wa vijiji vya Namagondo na Mulutima, wilayani Ukerewe.

Mwingine Omary Aman (10), mkazi wa Dar es Salaam aliyefia kwenye Kituo cha Afya Mriti na mfanyakazi wa mtumbwi huo
Paul Damas (35), mkazi wa Halwego, Ukerewe.

Habari zaidi toka eneo lingine la tukio kwenye Kisiwa cha Kamasi, zinadai miili watu wengine wawili waliokufa baada ya mtumbwi wenye namba RMB 2816, kupigwa na upepo karibu na Kisiwa
cha Mafunke, nayo imepatikana.

Miili iliyopatikana imetambuliwa kwa majina ya Matiku Marwa (50), na Nyauku Magabe (35), wote wakazi wa Kijiji cha
Bisumwi, Wilaya ya Musoma, mkoani Mara.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Bw. George Lukalagalila, alisema
watu hao walipatwa na dhoruba hilo saa tano asubuhi wakati
wakisafiri kutoka kisiwani humo kwenda Kisiwa cha Ghana. 

Maiti hizo zimehifadhiwa kwenye Kisiwa cha Kihala, ambapo mipango ya kuzisafirisha kwenda Musoma inaendelea.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ernest Mangu, alithibitisha kuwepo kwa matukio hayo na kuongeza kuwa, tayari Maofisa
wa jeshi hilo wamekwenda eneo la tukio kufanya uchunguzi.

No comments:

Post a Comment