26 February 2013

Saba wanaswa kwa ujambazi *Wakamatwa na bunduki ya kivita, risasi 53 *Wakili kuhusika na Tukio la mauaji Bukombe


Na Faida Muyomba, Geita

JESHI la Polisi mkoani Geita, linawashikilia watu saba wanaodaiwa kuwa majambazi akiwemo mfanyabiashara wa duka, mkazi wa Masumbwe, wilayani Mbogwe, wakiwa na bunduki ya kivita.


Kamanda wa Polisi mkoani humo, Leonard Paulo, alisema watu
hao walikamatwa Februari 22 mwaka huu, saa tano asubuhi katika
Kitongoji cha Shinyanga 'A' wilayani humo.

Alisema bunduki hiyo ilifichwa katika duka la mfanyabiashara ambapo jeshi hilo lilipata taarifa kuwa, watu hao walikuwa wakijianda kwenda kufanya ujambazi, wilayani Chato.

“Bunduki iliyokamatwa ni aina ya Uz-Gun, yenye namba ZM 10038, risasi 53 na magazini mbili ambayo ilifichwa kwenye duka
la mfanyabiashara anayeitwa Bw. Jamali Mabula (37), mkazi wa Tarafa ya Masumbwe,” alisema Kamanda Paulo.

Aliongeza kuwa, Bw. Mabula, alikiri hukusika na matukio mbalimbali ya ujambazi ndani na nje ya Mkoa huo pamoja
na kuwataja wenzake sita ambao amekuwa akishirikiana
nao katika matukio ya aina hiyo.

Watuhumiwa hao ni Masele Martine (35), mkazi wa Nansio wilayani Ukerewe, Cosmas Fabian (28), mkazi wa Masumbwe
na Billiani Silvanus (36), mkazi wa Tambukareli wilayani Geita.

Wengine Charles Kenedy(25), mkazi wa Shilabela wilayani Geita, Mahangaiko Katabalo (28), Luhende Bundala(37), ambao wote ni wakazi wa Lunzewe.

“Watuhumiwa wote walishiriki tukio la mauaji ya Joseph Paulo (48), Februari 15 mwaka huu, wilayani Bukombe, pia walikamatwa na simu mbili za mkononi aina ya Nokia zilizoporwa katika tukio hili.

“Mbali ya kujihusisha na matukio ya ujambazi, watuhumiwa hawa ni vinara wa matukio mbalimbali katika mikoa ya Mwanza pamoja
na Shinyanga,” alisema Kamanda Paulo.

Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani wakati wowote. Aliwaomba wananchi wote wa mikoa husika kudumisha ushirikiano na jeshi hilo kwa kufichua wahalifu.

No comments:

Post a Comment