08 February 2013

Maboma sita yachomwa moto katika mapigano


Na Mashaka Mhando, Korogwe

MABOMA sita ya wafugaji wa Kimang'ati yaliyopo katika vijiji
vya Gereza na Mkwakwani, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, yanadaiwa kuchomwa moto na kusababisha jamii hiyo kukosa
makazi baaada ya kutokea mapigano ya wafugaji na wakulima.


Mbali na tukio hilo, inaelezwa kuwa vyakula, kuku na mali nazo zimeteketea kwa moto ambapo wakulima kutoka vijiji hivyo, wamelazimika kuzihama nyumba zao wakihofia kukamatwa
na polisi waliofika kutuliza hgasia na kukamata wahalifu.

Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka kwa mkulima mmoja aliyepo mafichoni (jina tunalo), alisema vurugu hizo zilitokea juzi baada ya wafugaji wanaodaiwa kuhamia eneo hilo kuingiza ng'ombe wao katika mashamba yao na kula mazao yaliyokuwa shambani.

Mkulima huyo kutoka Kijiji cha Mkwakwani, alisema hali hiyo
ndio chanzo cha vurugu zilizotokea ambapo Jeshi la Polisi nalo linahusika kwa sababu ya taarifa wanazotoa kuzifanya mtaji.

“Mgogoro huu kati ya wakulima na wafugaji, umedumu muda
mrefu lakini kila tunapopeleka taarifa kwenye Kituo cha Polisi
Mnyuzi wanazifanya mtaji kwa kupindisha hazi za wakulima
na kuwapendelea wafugaji.

“Sisi tunaamini wenzetu wafugaji wanatoa chochote kwa polisi
ndio maana taarifa zetu hazifanyiwi kazi na kuonekana hatuna
haki sasa uvumilivu umetushinda na kuamua kuchoma moto
nyumba zao na kuua mifugo yao,” alisema mkulima huyo.

Mwandishi watu alishuhudia baadhi ya wafugaji wakiandikisha maelezo kwenye kituo Kidogo cha Polisi Mnyuzi wengine wakipewa fomu za PF3, ili waende kupatiwa matibabu
baada ya kujeruhiwa katika ugomvi huo.

Mkulima huyo aliongeza kuwa, licha ya wafugaji kuingiza ng'ombe katika mashamba yao, pia wamekuwa wakiwatisha wakulima na kutaka kuwapiga mishale ndipo wakulima wachache waliokuwepo shambani, waliwapigia simu wenzao na kuanza mapambano.

Alisema wakati vurugu hizo zikiendelea, polisi kutoka Korogwe walifika eneo hilo wakiwa na magari mawili aina ya Land Rover Difender, Toyota Land Cruiser na silaha za moto.

“Polisi walifanikiwa kutuliza vurugu ingawa walikuta maboma yamechomwa moto na baadhi ya mali zimeungua,” alisema.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Mrisho Gambo alipotafutwa kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana mara baada
ya simu zake kuzimwa ambapo Ofisa Tarafa ya Magunga,
Bw. John Kimweri, alikiri kutokea kwa tukio hilo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Constatine Masawe, alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa tukio hilo alisema kwa wakati huo yupo Handeni akiendelea na ziara ya kikazi na Mkuu wa Mkoa huo Luteni mstaafu Chiku Gallawa hivyo hakuwa na taarifa zozote.

1 comment:

  1. MAJI MAREFU AU STEVEN NGONYANI TUNAKUAMINIA UKITOKA BUNGENI WAHI KOROGWE ULIWAHI WANANCHI WALIPOKUWA WANACHOMANA MOTO NATUMAINI HILI HALITAKUSHINDA WEWE NI JEMBE

    ReplyDelete