08 February 2013

Auawa kikatili, anyofolewa sehemu za siri


Na Suleiman Abeid, Shinyanga

MAUAJI yanayochangiwa na imani za kishirikina, yameendelea kushika kasi mkoani Shinyanga, baada ya watu wasiofahamika kumuua kikatili mkazi wa Kijiji cha Igwamanoni, wilayani
Kahama Yunge Ngussa (65).

Akizungumza na Majira jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Evarist Mangalla, alisema baada ya mauaji hayo wahusika walikata sehemu za viungo vya marehemu na kuondoka navyo.

Alisema marehemu alishambuliwa na mtu au kundi la watu kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufa ambapo mauaji hayo yalitokea juzi kati ya saa tisa usiku na 11
alfajiri baada ya kuvamiwa nyumbani kwake.

“Marehemu aliumia vibaya sehemu za shingoni, kichwani hivyo kutokwa na damu nyingi iliyosababisha kifo chake na baadaye kunyofoa sehemu za siri, matiti na kuondoka navyo,” alisema.

Aliongeza kuwa, mauaji hayo yanahusishwa na imani potofu za kishirikina na hadi sasa, hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na
tukio hilo ambapo msako mkali unaendelea kuwatafuta wauaji.

Kamanda Mangalla ametoa wito kwa raia kutoa taarifa
ambazo zitafanikisha kukamatwa wauaji hao.

Katika tukio lingine, mwanafunzi wa darasa la pili aliyekuwa akisoma katika Shule ya Msingi Buduhe, wilayani Shinyanga,
Lega Charles (9), alikufa papo hapo baada ya kugongwa na
gari lililokuwa kwenye mwendo kasi.

Kamanda Mangalla alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa tano asubuhi katika Barabara ya Solwa-Salawe. Gari iliyosababisha kifo hicho ni Mitsubishi Fuso namba T 684 BEU, ambayo ilikuwa ikiendeshwa
na mkazi wa Magu, mkoani Mwanza, Bw. Daniel Simo (30).

Alisema chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva katika eneo la makazi ya watu ambaye baada ya kubaini ameua, alikimbia na hivi sasa anatafutwa na polisi ili aweze kufikishwa mahakamani kujibu shitaka la kusababisha kifo hicho.

No comments:

Post a Comment