18 February 2013
Kesi ya mbunge Bahi kusikilizwa mfululizo
Na Rehema Mohamed
KESI ya kuomba na kupokea rushwa ya sh.milioni 8 inayomkabili Mbunge wa Bahi (CCM) Bw.Omary Badwell itaendelea kusikilizwa Februari Machi mosi mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbele ya Hakimu Hellen Liwa,jana kesi hiyo ililetwa kwa ajili ya kusikilizwa,lakini ilishindikana kwa sababu wakili wa mbunge huyo kushindwa kufika mahakamani hapo kwakuwa anaumwa.
Wakili wa serikali kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Bi.Lizzy Kiwia aliieleza mahakama hiyo kuwa walikuwa na mashahidi wawili aliokuja kutoa ushahidi wao.
Mashahidi hao ni Bw.Crasco Mataika na Bw.Amani Madede ambao Hakimu Liwa aliwaonya na kuwataka wafike mahakamani hapo Machi mosi kesi itakapokuja kusikilizwa.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka 2012, katika maeneo tofauti ya jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alivunja kifungu cha 15 (1) (a) cha Sheria namba 11 ya Makosa ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Ilidaiwa siku ya tukio, mshitakiwa akijua kuwa ni kosa kisheria, alishawishi apewe Sh. milioni 8 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana.
Ilidaiwa kuwa, Badwel aliomba rushwa hiyo ili awashawishi wajumbe wa kamati yake kupitisha hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Katika shitaka la pili inadaiwa kuwa,Juni 2 mwaka 2012 katika Hoteli ya Peacock, iliyopo Ilala, Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alipokea rushwa ya Sh. milioni moja kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.
Ilielezwa kuwa lengo la rushwa hiyo lilikuwa ni kuwashawishi wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kupitisha hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment