05 February 2013

Kashasheki kuzindua kituo cha wageni WMA Burunge



Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Marekani Bw. David Hayes, leo watazindua Kituo cha Wageni cha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA), cha Burunge, mkoani Manyara.

Uzinduzi huo ni sehemu ya maadhimisho ya Jumuiya za WMA zilizoanzishwa nchini mwaka 1998 kwa mujibu wa sheria ya wanyamapori na kukikabidhi kwa wananchi.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Wizara hiyo, Bw. George Matiko, ilisema ujenzi wa kituo hicho ni mafanikio ya programu ya kuendeleza WMA inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani.

“Uzinduzi huu ni ishara kuwa, Serikali ya Marekeni itaendelea kuunga mkono shughuli za uhifadhi nchini pamoja na mapambano dhidi ya ujangili,” alisema Bw. Matiko.

Kituo cha Wageni cha Burunge ni sehemu ya misaada inayotolewa na Serikali ya Marekani katika programu ya WMA nchini kote.

Misaada mingine iliyotolewa na WMA kwenye kituo hicho ni
ujenzi wa barabara za kufanikisha uhifadhi, kituo cha askari wa Wanyamapori na kujenga lango kuu la kuingilia kwenye eneo la jumuiya hiyo.


Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori ni maeneo ya wanyamapori yanayohifadhiwa na kulindwa na wananchi kwa manufaa yao na Taifa ambapo WMA 17 zilizopo nchini, zimesajiliwa rasmi na wahusika kuruhusiwa kufanya matumizi endelevu.

Bw. Matiko alisema, pia kuna maeneo 21 ambayo yako katika
hatua mbalimbali za kuanzishwa WMA.

No comments:

Post a Comment