05 February 2013

Jaji Mkuu: Kuchelewa upepelezi kunachangia mlundikano wa kesi


Gladness Theonest na Neema Malley

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, amesema mahakama nyingi nchini, bado zinakabiliwa na changamoto ya msongamano wa kesi ambapo sababu moja wapo inayochangia
hali hiyo ni kuchelewa kwa upelelezi wa kesi.

Changamoto hiyo inachangia msongamano wa wafungwa katika Magereza mbalimbali nchini ambapo watuhumiwa wanapotakiwa kupeleka mashahidi, hawatekelezi ahizo hilo kwa wakati.

Jaji Othman aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maadhimisho
ya Siku ya Sheria nchini inayotarajia kufanyika kesho.

Alisema sababu nyingine ni mahakama kuwa na kesi nyingi
ambazo hazisikilizwi kwa kipindi kinachotakiwa.

“Ili tuweze kuondokana na msongamanao wa wafungwa gerezani, ushirikiano kati ya vyombo mbalimbali unahitajika kwani dhamira ya mahakama ni kuharakisha kesi, kuhakikisha wafungwa hawakai mahabusu muda mrefu,” alisema.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Jaji Othman alisema mwaka
huu watazungumzia mambo muhimu yanayojenga dhana ya utawala bora, umuhimu wa utawala wa sheria nchini na wajibu wa kila mtu kuheshimu utawala wa sheria.

Alisema mgeni rasmi katika maadhimisho hayo atakuwa Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine watakaokuwepo ni Spika wa
Bunge Bi. Anne Makinda, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Mkaungu, Waziri wa Katiba na Sheria, Bw. Mathias Chikawe na Naibu wake Bi. Angela Kairuki.

Sherehe hizo zitafanyika katika vituo vya ngazi zote za mahakama nchini isipokuwa kwenye mahakama za mwanzo ana kauli mbiu inasema “Utawala wa sheria, Umuhimu na Uimarishaji wake nchini”.

No comments:

Post a Comment