05 February 2013

Kanda ya Ziwa waunga mkono kauli ya Shibuda


Na Jesca Kileo

BAADHI ya wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, wameunga mkono kauli ya Mbunge wa Maswa Magharibi, Bw. John Shibuda kuwa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepoteza mvuto kwa wananchi waishio kanda hiyo.


Kauli ya wananchi hao imekuja siku chache baada ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa kudai chama hicho bado kinakubalika na wananchi wa mikoa hiyo.

Dkt. Slaa alipuuza madai ya Bw. Shibuda aliyedai kuwa, chama hicho hakiaminiki tena na wananchi wa Kanda ya Ziwa.

Wakizungumza na Majira Dar es Salaam hivi karibuni, wananchi hao walisema kauli ya Bw. Shibuda ina ukweli ndio maana chama hicho kimeshindwa vibaya katika chaguzi ndogo zilizofanyika mwishoni mwa 2012.

“Uongozi wa CHADEMA kama utathubutu kumfukuza Bw. Shibuda, kwa sababu ya kusema ukweli tutafanya maandamano maandamamo makubwa ya wananchi wa kanda hii.

“Viongozi wa chama hiki wameshindwa kutekeleza matakwa ya wananchi badala yake wamekuwa wakiendeleza propaganda na kuwafukuza watu wanaowapinga kwa hoja,” walisema.

Bw. William Machimu, alisema kipimo cha kuporomoka kwa CHADEMA ni uchaguzi mdogo wa marudio uliofanyika kwenye baadhi ya kata ikiwemo Bugalama, wilayani Kahama ambapo
CCM ilipata kura 1,300, CHADEMA 700 na TADEA 147.

Kata ya Mwawaza, CCM kura 1,500, CHADEMA 800 na TADEA 28 ambapo Kata ya Lubili, wilayani Misungwi CCM ilipata kura 1,200, CHADEMA 700 na TADEA 28.

Alisema katika Uchaguzi Mkuu 2010, waliipokea CHADEMA vizuri wakiamini itawasimamia na kutetea masilahi yao
lakini hali hiyo imekuwa tofauti na walivyotarajia.

No comments:

Post a Comment