18 February 2013
BTL yapania kutwaa tuzo uandishi mahiri
Na David John na Goodluck Hongo
KAMPUNI ya Business Times Limited (BTL), inayochapisha magazeti ya Business Times, Majira na Spoti Starehe, imeshika nafasi
ya tatu kwa kuwasilisha makala, habari na picha ambazo zitashindaniwa katika Tuzo za Uandishi wa Mahiri wa Habari nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Katibu Mtendaji wa Baraza la habari (MCT) Bw. Kajubi Mukajanga alisema kazi zilizopokelewa ni 946 na Kampuni ya Business Times imepeleka kazi 91 nakushika nafasi ya tatu na huku kukiwa na makundi 19 yatakayoshindanishwa.
Alisema katika mashindano ya mwaka huu tuzo tatu mpya zimeingizwa ambazo ni Tuzo ya Kilimo na Biashara ya Kilimo mpiga picha bora wa luninga na tuzo ya afya ya uzazi kwa vijana ambapo tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 2009 kumekuwa na ongezeko kubwa la kazi za waandishi ili ziweze kushindanishwa.
Bw. Mkajanga alisema kuwa kamati imepokea kazi 660 kutoka magazetini,kazi 286 kutoka redio na luninga ambapo Mkoa wa Dar es Salaam ndio ulioongoza kwa waandishi wengi kupeleka kazi zao kwa nje ya Dar es Salaam Mkoa wa Morogoro ndio uliokuwa ukiongoza kupeleka kazi nyingi lakini safari hii haupo kabisa.
"Kampuni ya Business Times imeshika nafasi ya tatu kwa waandishi wake kuleta kazi zao hapa kwa ajili ya kushindania tuzo za Umahiri katika Uandishi wa Habari kwa mwaka huu ambapo hii inaonesha ni jinsi gani mashindano haya yanavyoaminika tangu yalipoanzishwa na mwaka huu mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Mohamedi Shein,"alisema Mkajanga
Alisema jopo la majaji 10 litaanza kazi yake Februari 25 mwaka huu, ambapo kilele chake kitakuwa ni Aprili 5,2013 na jopo hilo litaongozwa na Bw.Wenceslaus Mushi huku wengine wakiwa ni Dina Chahari,Yusufu Chunda,Anaclet Rwegayura,Pudensiana Temba,Ngalimecha Ngayoma,Pili Mtambalike,Mwanzo Milinga Atilio Tagalile na Bi. Edda Sanga.
Alifafanua zaidi kuwa wakati hayo yakiendelea jopo la wataalamu wa Tuzo ya Maisha ya Mafanikio katika Tasnia ya habari mwaka 2013 linaendelea na kazi hiyo ambapo linaongozwa na Theophil Makunga akiwemo pia Bi.Joyce Mhavile, Lilian Kallange,Jenerali Ulimwengu na Hamis Mzee.
Makundi ya tuzo hizo ni Utawala Bora,Uchumi na Biashara,Michezo na Utamaduni,Mazingira,Afya,Virusi vya Ukimwi na Ukimwi,Malaria,Watoto na Elimu,Utalii na Uhifadhi,Majanga,Afya ya Uzazi kwa Vijana Mpiga Picha Bora,wa Luninga,Mchora Katuni Bora,Mpiga Picha Bora wa Magazeti,Biashara na Kilimo na kundi la wazi ambapo halipo katika makundi yote yaliyotajwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment