28 January 2013

Zitto amtaka Sitta kufikiria upya chama cha kugombea urais


Na Gladness Mboma

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe amesema, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Sumuel Sitta ana haki ya kugombea nafasi ya urais kama ilivyo kwa Mtanzania mwingine, lakini anapaswa kufikiria upya kuhusu chama anachotaka kupeperusha bendera ya urais.


Hata hivyo Bw. Zitto alisema wagombea wote wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wafahamu kuwa wanapoteza muda kwa kuwa Rais wa mwaka 2015 atatoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kauli hiyo ya Bw. Zitto ilitokana na gazeti ili kutaka atoe maoni yake kuhusiana na kauli ya Waziri huyo ya kutaka kugombea urais mwaka 2015 iwapo dhamira yake itaridhika na mazingira ya upepo wa kisiasa kwa wakati huo, ambapo aliitaadharisha CCM kwamba wasipoangalia Rais atatokea upinzani.

Bw. Zitto alisema wagombea wa CCM wanapaswa kufahamu kuwa wanapoteza muda kwa kuwa Watanzania wamekichoka chama hicho na hawawezi kukipa tena fursa ya kuongoza.

"Kwa hali ya sasa ya siasa za nchi na namna ambavyo Watanzania wamechoka itakuwa ni ajabu sana kwa CCM kushinda Uchaguzi Mkuu 2015, hivyo watu kama wakina Waziri Sitta wanaotaka kuongoza nchi ni vema wakafikiria upya kuhusu chama wanachotaka kupeperusha bendera,"alisema.

Alisema hivi sasa nchi inahitaji kiongozi ambaye siyo tu anataka madaraka ya uongozi, bali pia anayetaka kuleta mabadiliko makubwa, kuanzia kifikra mpaka kiutendaji.

"Mtu huyo ni lazima atoke chama chenye kuaminiwa na wananchi na chama hicho kwa kweli ni CHADEMA kwa sasa,"alisema.

Bw. Zitto alisema Watanzania wanataka kiongozi ambaye atatoa majawabu ya changamoto za nchi, kwani nchi inakumbana na misukosuko ya kuongezeka kwa migawanyiko inayotokana na udini na hata vyama.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Bw. Nape Nnauye akitoa maoni yake alisema kuwa alichozungumza Waziri Sitta ni maoni yake mwenyewe na ana haki ya kuzungumza kama ilivyo kwa Watanzania wengine.

Awali Waziri Sitta akizungumza katika mahojiano maalumu na chombo kimoja cha habari kinachotoka kila siku alitaja mambo kadhaa aliyoeleza kuwa ni ishara ya kukubalika kwake ikiwamo kuteuliwa na marais wote wanne katika nyadhifa mbalimbali ikiwemo uwaziri.


No comments:

Post a Comment