28 January 2013

Ni mapambano tena Dar,Moro *WANANCHI WACHOMA MAGARI,WAPORA,WAVUNJA NYUMBA *RC,DC WADAIWA KUWA CHANZO,MMOJA AFA *DAR,POLISI MACHINGA WAPAMBANA



Na Waandishi Wetu Dar, Kilosa

WANANCHI wenye hasira katika Kijiji cha Dumila, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro walifanya vurugu kubwa zilizoambatana na wizi, uporaji na uharibifu wa mali, ambapo nyumba mbili za kulala wageni zilivunjwa na magari kadhaa kuharibiwa kwa kupigwa mawe na mtu mmoja kufariki dunia kwa mshtuko wa mabomu.


Wakati vurugu hizo zikiendelea wilayani Kilosa,Dar es Salaam maeneo ya Kariakoo kulizuka vurugu kubwa zilizosababisha maduka kufungwa na watu kukimbia hovyo baada ya askari wa jiji kutaka kumkamata mfanyabiashara (machinga) na askari polisi kuingilia kati.

Katika vurugu zilizotokea wilayani Kilosa ziliibuka kuanzia saa 2 asubuhi, ambapo mamia ya wananchi wa kijiji hicho walianza kuzuia magari kupita kwa kuweka magogo ya miti, mawe na kuwasha matairi ya magari barabarani wakipinga kauli ya Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Bw. Elias Tarimo kukitangaza kitongoji cha Mabwegele kuwa ni kijiji na kuzuia wananchi wa Dumila kuendelea na shughuli za kilimo katika kijiji hicho.

Katika vurugu hizo, mkazi mmoja Bw. Mohamed Msigala (67) alipoteza maisha kutokana na mshutuko uliosababishwa na milipuko ya mabomu ya machozi yaliyokuwa ya kipigwa kuwafurusha waandamanaji hao.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro Bw. Faustine Shilogile alisema wananchi hao walivunja nyumba hizo za kulala wageni ambazo zinamilikiwa na watu wa jamii ya Kimasai na kuiba vitanda, magodoro, shuka na taulo.

Kuhusiana na vurugu hizo, Kamanda Shilogile alisema watu 19 walikamatwa na kuhojiwa na polisi  kisha kuachiwa kwa dhamana na kwamba uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Kamanda Shilogile alisema chanzo cha vurugu hizo ni tangazo la mkuu wa wilaya ya Kilosa Bw. Tarimo alilolitoa juzi katika kitongoji cha Mabwegele kwamba kitongoji hicho ni kijiji na kupiga marufuku shughuli za kilimo katika eneo hilo, tamko ambalo lilipingwa na wananchi hao na kuamua kufanya vurugu hizo.

Akizungumza na gazeti hili Mkuu huyo wa wilaya alidai Mahakama ilikipa kitongoji hicho hadhi ya kijiji na kwamba vurugu hizo zinachochewa na viongozi wa vijiji jirani kwa lengo la kujinufaisha.

Akizungumza na wananchi hao jana katika eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Joel Bendera alitofautiana na mkuu wa wilaya pale alipowaambia wananchi hao kwamba, Mabwegele ni kitongoji na wala hakijawa kijiji huku akiwahimiza kuendelea na shughuli zao za kilimo kama kawaida.

" Mabwegele ni bado ni kitongoji pamoja na mahakama kukipa hadhi ya kijiji tambueni sheria na haki ni vitu viwili tofauti, kwa haki Mabwegele ni kitongoji na ninawaambia, endeleeni na shughuli zenu za kilimo katika kitongoji hicho hakuna mtu yeyote atakayekuja kuwabughudhi," alisema Bendera

Kitongoji cha Mabwegele ni eneo ambalo linakaliwa na wafugaji wa jamii ya Kimasai lakini wananchi wa kijiji cha Dumila wana mashamba yao katika eneo hilo na uendesha shughuli za kilimo katika mashamba hayo.

Jamii hiyo ya wafugaji miaka zaidi ya 10 iliyopita ilipeleka mashitaka mahakamani kudai kumilikishwa eneo hilo na kupewa hadhi ya kijiji na mahakama kukubaliana na kukipa kitongoji hicho hadhi ya kijiji hali iliyozua ugomvi na kutoelewana kati ya pande hizo mbili.

Naye mkazi mmoja wa kijijini hapo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini ameiomba serikali kutoa ufafanuzi kuhusiana na mgogoro huo kwa kuwa wananchi wanahishi kwa hofu, kwani wahusika wa vurugu wametamba kurejea tena kuvunja nyumba na kuharibu mali.

"Sasa hivi sisi tunaishi kwa hofu kubwa hatujui wataanzisha tena vurugu muda gani, kwani tunaogopa hata kulala majumbani mwetu usiku kuhofia kuchomwa moto tukiwa tumelala,"alisema.

Wakati huo huo, Dar es Salaam kumetokea vurugu kubwa katika maeneo ya Kariakoo kati ya askari wa jiji (mgambo) na askari wa Jeshi la Polisi, baada ya machinga kudaiwa kutaka kumnyang'anya silaha askari polisi.

Vurugu hizo ambazo zilidumu kwa nusu saa zilitokea mchana na kusababisha askari wawili wa jiji kujeruhiwa vibaya, huku ikidaiwa pia askari mmoja wa jeshi la polisi PC Khalid mwenye namba G,6578 naye alijeruhiwa katika vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala,Marietha Minangi akizungumzia vurugu hizo kwa waandishi wa Habari alisema hali hiyo ilitokana na mgambo wa jiji kumkamata mfanyabiashara mmoja,ambapo askari polisi aliingilia kati jambo ambalo lilizua vurugu.

"Hali hiyo ilisababisha wafanyabiashara wengine kupandwa na jazba na kisha kumfuata askari na kutaka kumnyang'anya silaha kwa nia ya kuwajeruhi mgambo hao,"alisema Kamanda.

Alisema wakati wanaendelea kuchunguza chanzo cha vurugu hizo wafanyabiashara walimkamata askari polisi kwa lengo la kutaka kumnyang'anya silaha, lakini walifanikiwa kukamatwa na kupelekwa Kituo Kidogo cha Polisi Msimbazi.

Wakati vurugu hizo zikitofanyika, baadhi ya wafanyabiashara walilazimika kufunga biashara kwa kuhofia mali zao kuporwa, hata hivyo polisi walifika katika eneo hilo na kuimarisha hali ya ulinzi na amani.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, vurugu hizo zinatokana na askari wa jiji kuendeleza vitendo vya rushwa kwa wafanyabiashara wadogowadogo, ambapo wamekuwa wakichukua sh. 500 kwa kila machinga wa mwanvuli na baadaye kwenda kuwafukuza, jambo ambalo linasababisha vurugu.

Habari hii imeandikwa na Masau
Bwire,Aneth Kagenda na Gifti Mongi.

 

No comments:

Post a Comment