21 January 2013

ZECO yaaswa kutoa huduma bora



 Na Mwajuma Juma, Zanzibar

UONGOZI wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO)limeaswaa kuwa makini katika taratibu zake za kutoa huduma bora kwa lengo la kupunguza kero na lawama kutoka kwa wateja wa huduma hiyo.


Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi ya kukagua matengenezo ya kituo cha kusambazia Umeme katika eneo la Mji mkongwe hapo Darajani ambacho kilipata hitilafu ya umeme na kusababisha kukosekana kwa kuduma hiyo kwa karibu saa 24.

Balozi Seif alisema matumizi ya huduma za umeme hivi sasa yameongezeka mara dufu Nchini, hivyo Shirika la Umeme iwapo halitakuwa makini katika kukabiliana na ongezeko hilo lawama zaidi zitaendelea kulipata shirika hilo.

Aliuagiza uongozi wa shirika hilo kupitia Waziri wake kufanya utaratibu wa kuyawasilisha yale matatizo ambayo hayamo katika uwezo wao na serikali kwa upande wake itajaribu kutafuta mbinu ya kuyatatua.

"Uongozi wa Shirika lazima uelewe kwamba matumizi makubwa ya huduma za umeme yameongezeka zaidi kiasi ambacho kinaonekana kuleta changamoto kwa shirika hilo," alisema.

Aliwaagiza wahandisi wa shirika hilo kufanya kazi ya ziada hasa wakati wa kukabiliana na hitilafu za umeme zinapojitokeza katika sehemu mbali mbali hapa nchini.

Mapema Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Bw. Hassan Ali alimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wahandisi wa shirika hilo wamelazimika kuongeza mtandao wa Umeme katika eneo hilo ili kupunguza hitilafu inayojitokeza kila mara katika kituo hicho.

Bw.Hassan alifahamisha kwamba mtandao uliopo hivi sasa ndani ya eneo lote la mji Mkongwewa Zanzibar tayari umeshaonyesha dalili ya kuzidiwa na wateja kutokana na kukua kwa matumizi ya huduma hiyo
muhimu.

Kituo cha kusambazia huduma ya umeme ndani ya Mji Mkongwe kilichopo Darajani Mjini Zanzibar kimekuwa kikikabiliwa na hitilafu ya mara kwa mara ya umeme la kusababisha usumbufu wa kukatika katika kwa umeme
katika eneo hilo.



No comments:

Post a Comment