15 January 2013

Wavamizi pori Mbangara watiwa mbaroniNa Esther Macha,
Mbeya

WATU watano jamii ya wafugaji wanashikiliwa na Polisi Wilayani Chunya mkoani Mbeya wakituhumiwa kuwashawishi wafugaji wenzao kuwavamia maofisa wa Halmashauri hiyo waliokowa wakiendesha zoezi la kuwaondoa wafugaji waliovamia hifadhi ya misitu katika pori la Mbangara wilayani humo.

Wafugaji hao walikamatwa  juzi baada ya Maofisa hao kwenda msituni huko kwa ajili ya kuwaondoa wavamizi lakini waliokutwa walionekana kuwasiliana na wenzao kwa lugha ya Kimang'ati hali ambayo ilisababisha kundi la Morani zaidi ya 40 wakiwa na silaha za jadi kuvamia msafara wa viongozi hao ambao walikuwa ni Maofisa Mifugo, Misitu, Polisi, Mgambo na waandishi wa habari.


Waliokamatwa katika oparesheni hiyo walitambuliwa kwa majina ya Shija Ndagi, Yonza Polisi, Mwang'ola Sihanga, Julius Rangai na Juma Petro ambao wote ni wafugaji na ambao walikutwa wakiwa katika eneo la tukio huku wakiwa na simu za mkononi pamoja na silaha nyingine za jadi.

Hata hivyo kutokana na operesheni hiyo wafugaji hao ambao  walionekana kukamatwa mifugo yao walijikusanya kisha kuvamia kundi la askari na wataalamu waliokuwa kwenye kazi hiyo wakiwa na mikuki na mishale kwa lengo la kuikomboa mifugo yao hali ambayo walifanikiwa kuondoka na mifugo hiyo kwa kile kilichodaiwa na kiongozi wa msafara huo kuwahurumia ili waondoke kwa amani.

Akizungumza na waandishi wa habari katika operesheni ya  kuwahamasisha wafugaji hao,Kiongozi wa msafara huo,Patrick Chonya alisema kuwa licha ya kutoa taarifa kwa  viongozi wa Serikali ya kijiji cha Mbangala pamoja na  watalaamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya  kuwaelimisha  wafugaji kuhama hawajafanya hivyo hali iliyosababisha kutuma kikosi cha watalaamu na askari polisi na mgambo kuwahamisha kwa nguvu.

“Bado tunaendelea na zoezi  hili  kwa nguvu zote ili kunusuru uharibifu wa mazingira unaoendelea kufanyika katika bonde hili, lakini pia bado tunaendelea kutoa elimu kwa wafugaji”alisema.

Kwa mujibu wa Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Chunya ,Benedict Matogo alisema wanyama hao wakikamatwa katika operesheni yoyote wamiliki watatozwa faini kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na baraza la Madiwani wa Halmashauri ambapo kila mfugo hutozwa faini ya Shilingi 20,000 kwa kila mmoja.

No comments:

Post a Comment