15 January 2013

Serikali yakiri haijatenga ardhi ya kilimo, ufugajiNa Peter Mwenda

SERIKALI imekiri kuwa haijatenga ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji kama ilivyotengwa kwa ajili ya wanyama pori.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Bi.Sophia Kaduma akizungumza katika warsha ya siku moja ya kuendeleza kilimo nchini iliyofanyika Dar es Salaam juzi alisema serikali imegendua kasoro hiyo na inafanyia kazi ili kukuza kilimo nchini.

"Nakubaliana nanyi kuwa nchini Tanzania hakuna ardhi iliyotengwa rasmi kwa ajili ya kilimo kama ilivyo katika sekta nyingine ya madini, misitu,wanyama pori, sisi tupo katika mchakato wa kuanzisha sheria itakayolinda ardhi kwa ajili ya kilimo" alisema Bi. Kaduma.

Alisema pia ardhi ya uwekezaji imeanza kupatikana inayosimamiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)na tayari zimetengwa mashamba kuanzia 5,000 hadi 60,000.

Bi.Kaduma alisema serikali imejipanga kuongeza utoaji elimu kwa wakulima kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambayo inashusha kiwango cha uzalishaji wa mazao.

Alisema Serikali imejipanga kuimarisha miundombinu ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ili kupunguza mfumuko wa bei kwa mlaji.

Katika warsha hiyo iliyoandaliwa na Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) kwa wadau wa kilimo nchini, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw.Salum Shamte alisema Serikali inawapunguzia ari ya wakulima kutokana na kupanda kwa kodi nyingi za mazao zinazopandishwa kiholela.

Alisema wakulima wanalipa kodi mara 17 wakati wenye viwanda hawalipi chochote wakati hiyo ndiyo sekta inayobeba maisha ya watanzania zaidi ya asilimia 80.

Ofisa Ardhi Mwandamizi wa Wizara ya Ardhi,Nyumba  na Maendeleo ya Makazi, Bi. Jane Kapongo alisema wizara haigawi ardhi bali inasimamia sheria ambazo idara mbalimbali za manispaa ambazo zinawajibika kugawa ardhi.

Naye Mhadhiri katika Idara ya Ugani Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Profesa Deogratias Rutatora alisema sekta ya kilimo ndiyo pekee inavusha taifa kutoka katika umasikini na kuwataka wakulima wajitambue kuwa wanahitajika kulima kwa bidii ili kujikomboa.

No comments:

Post a Comment