21 January 2013
Watanzania watakiwa kutii mamlaka zilizopo serikali
Na Florah Temba,
Moshi
WATANZANIA wametakiwa kujituma katika kazi ikiwa ni pamoja na kutii mamlaka zilizopo katika serikali na hata kwenye dini, hatua ambayo itasaidia kudumisha amani na mshikamano ulioachwa na hayati mwalimu
Julius Kambarage Nyerere.
Mbali na hilo wametakiwa pia kuondoa mtazamo kuwa wakuu wa wilaya hawana kazi na kutambua kuwa wana majukumu mazito katika nchi ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama.
Wito huo umetolewa jana na Captain David Nickol mzee wa karne ya sita ambaye alikuwa mkuu wa wilaya enzi za ukoloni kabla ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, ambapo alisema amani iliyopo nchini Tanzania ni msingi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hivyo inapaswa kuenziwa.
Bw.Nickol aliyasema hayo wakati akiweka shada la maua kwenye mnara uliopo YMCA mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, kuwakumbuka askari mashujaa waliopigana vita kuu ya pili ya dunia mwaka 1939 hadi mwaka 1945 na vita ya kumuondoa Idd Amin mwaka 1978 hadi mwaka 1979.
Alisema nchi ya Tanzania toka zamani imejulikana kama nchi ya utulivu na amani na kwamba Hayati Julius Kambarage Nyerere alisisitiza vitu hivyo enzi za uhai wake, hivyo ni vema watanzania wote wakasimama kupigania hilo ili kuweza kuepuka vurugu.
“Ninachoweza kusisitiza ni kwamba watanzania wafanye kazi hata wakifikisha miaka 80 na kuitii serikali, kanisa na hata misikiti,kwani Tanzania hakuna chuki,ugomvi wala vurugu na hili ni kutokana na misingi aliyoiacha mwalimu Nyerere”alisema.
Katika hatua nyingine alisisitiza kuwa wakuu wa wilaya wanakazi kubwa na bado wanahitajika katika nchi, hivyo ni vema
watanzania wakaondokana na mitazamo kuwa waondolewe na nafasi hizo
zifutwe.
Bw.Nickol ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya katika maeneo mbalimbali hapa nchini enzi za ukoloni na kuhitimisha kazi hiyo mwaka 1961 wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ni mmoja wa wapiganaji katika
vita kuu ya pili ya dunia mwaka 1939 hadi mwaka 1945.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment