21 January 2013

Teknolojia Mbola kusambazwa nchini kuondoa umaskini



Na Moses Mabula, Uyui

WAZIRI wa Fedha Dkt Wlliam Mgimwa amesema Serikali
inaangalia uwezekano wa kusambaza teknolojia na mbinu zilizotumika katika kijiji cha millennia cha Mbola mkoani Tabora, zitumike katika vijiji vingine
hapa nchini.


Dkt Mgimwa, ameyasema hayo katika kijiji cha
Ilolangulu wilaya ya Uyui wakati akifungua Zahanati ya kijiji hicho ambayo hadi kukamilika kwake imegharimu kiasi cha shilingi milioni 49.

Alisema lengo la kusambaza teknolojia hiyo ni kuweza kutokomeza umaskini kwa haraka na kutimiza malengo 8 ya milenia.

Alisema kwamba ni vema wananchi wakahakikisha miradi
yote iliyotekelezwa chini ya mradi wa vijiji vya millennia mbola inatunzwa vizuri ili iwe daraja la kufundishia vijiji vingine nchini katika utekelezaji
wa malengo 8 ya milenia .

Waziri Mgimwa, amefika kijiji hapo kwa ajili ya
kujifunza na kujionea jinsi mradi huo shirikishi wa kijiji cha Milenia unavyooendeshwa na Umoja wa Mataifa ulivyoweza kupambana na umaskini kwa
wakazi wa vijiji 16 vya wilaya ya Uyui.

Awali Mratibu wa Mradi wa Kijiji cha Milenia cha Mbola mkoani Tabora, Dkt.Gerson Nyadzi, alisema wakazi wa kijiji hicho wameweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo baada ya kuwezeshwa na serikali.

Alisema kuwa mradi wa kijiji hicho umepewa pembejeo ili kuweza kuondokana na umaskini uliokithiri, ambapo wakulima wanavuna zaidi ya magunia 20 hadi 40 kwa heka moja ya mahindi.

Mapema Mwenyekiti wa kijiji cha Ilolangulu Ali Magoha alisema kuwa mradi huo umefanikiwa kutimiza malengo yote 8 yaliyokusudiwa kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 85.

Alitaja manufaa ambayo wameweza kupatikana ni pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa za matofali ya kuchoma na bati,uzalishaji wa mazao ya chakula
umeongezeka.

Pia alisema kwamba mradi huo umesaidia kupunguza
tatizo la vifo vya watoto chini ya miaka 5 na vifo vya akina mama wajawazito.

Alisema awali vifo hivyo vilikuwa wastani wa
watoto 3 nadi 5 katika kipindi cha miezi mitatu na kinamama 5 kwa kila mwezi lakini kwa sasa wastani huo ni kwa kipindi cha miezi 6 na wakati mwingine
hakuna kabisa.

Magoha alisema kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya
wananchi kupata elimu juu ya kutumia vyandarua na kuua mazalia ya mbuhivyo kupunguza kasi ya maradhi yan malaria katika eneo hilo..









No comments:

Post a Comment