14 January 2013

Wasabato wataka Katiba itoa uhuru wa kuabudu


Na David John

KANISA la Wasabato nchini (CDA), jana limetoa mapendekezo yake kwa Tume ya Katiba na kutaka Katiba ijayo itoe nafasi kwa dini zote nchini kuheshimu siku zao za kuabudu na waumini
wao kupewa siku za mapumiziko tofauti na ilivyo sasa.


Mchungaji wa kanisa hilo, James Machange, aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya kuwasilisha maoni yao akitolea mfano siku ya Jumamosi ndiyo wanayofanya ibada lakini baadhi ya waumini kama wanafunzi hawapati fursa ya kuabudu.

“Wakati mwingine hulazimika kwenda shule na wengine kazini jambo ambalo linanyima uhuru wa kuabudu, makundi madogo ya dini hayapewi nafasi ya kutambulika serikalini hivyo Katiba ijayo itoe fursa sawa kama ilivyo kwa makundi makubwa,” alisema.

Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, limependekeza Katiba ijayo itamke wazi kuwa siku ya Ijumaa
iwe mwisho wa kufanya kazi na si vinginevyo ili kutoa fursa
kwa Waislamu kushiriki ibada.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Musa Kundecha, alisema katiba ijayo iwe na kipengele kinachoitambua siku hiyo kuwa ya mapumziko na kutoa uhuru wa kila dini kutoa elimu inayohusu imani zao pamoja na kutambuliwa na Serikali.

“Elimu hii itolewe kulingana na maelekezo ya dini zao ili kuwaandaa waumini waweze kumcha Mungu, pia Katiba ijayo
itoe nafasi ya kuruhusu Muungano wa Serikali tatu ili kumaliza malumbano yanayojitokeza juu Muungano uliopo,” alisema.

Aliongeza kuwa, yapo maneno mengi yanayosemwa kuhusu Muungano hivyo Katiba itoe fursa ya kuazishwa Serikali hizo
ili kumaliza malumbano yanayoendelea hadi sasa.

No comments:

Post a Comment