28 January 2013

Wananchi watakiwa kujenga nidhamu TemekeNa David John

MKUU wa wilaya ya Temeke Sophia Mjema amewataka wananchi wa  wilaya hiyo kujenga nidhamu ya kusimamia vizuri huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya maeneo yao.


Alisema kama kunatokea uharibifu wa huduma ni vema wananchi wakarudi kwa serikali yao kwa ajili ya kuona namna gani huduma hizo zinaweza kushughulikiwa kwa haraka na huku wananchi wenyewe wakionyesha mstari wa mbele katika kuisaidia serikali si vinginevyo.

Akizungumza Dar es salaam jana mbele ya waandishi wa habari Mjema alisema Serikali inajitahidi katika kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi wake, lakini wakati mwingine wanashindwa kuonyesha ushirikiano kwa serikali katika kusimamia huduma hizo.

Akitolea mfano huduma za visima ambavyo vinajengwa na Serikali Mjema alisema  wananchi wanashindwa kuwa na usimamizi mzuri wa kuangalia miradi hiyo ndiyo maana hata vitu vidogo vidogo vinapo haribika wanakimbilia halmashauri au kutoa lawama kwa serikali.

Alisema kinachotakiwa wananchi wajenge utaratibu wa kulinda mali zao na kila mtu kuwa mlizi wa mwingine pindi anapoonekana kutaka kufanya uharibifu wa kitu fulani ambacho kipo kwa ajili ya maendele yao.

Aliongeza kuwa anatambua kuwa ndani ya Wilaya yake kuna changamoto kubwa ya maji, hivyo mbali na serikali kuchimba visima vingi lakini kuna maeneo mengine visima hivyo havitoi maji lakini wao kama halmashauri wanafanya kila jitihada ili kuona wananchi wake wanapata huduma hiyo muhimu pia ikiwa ni moja ya njia ya kutimizi ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM kuwa hakuna atakaye kufa kwa ajili ya kukosa maji.

Akizungumzia changamoto katika upande wa elimu alisema kero kubwa katika eneo hilo ni upungufu wa thamani ,madawati ,pamoja na vyumba vya madarasa hivyo mbali na serikalin kushuguhulikia changamoto hizo lakini si dhambi wananchi kama watashiriki kikamilifu ili kuondoa tatizo hilo.

Alisema Wilaya hiyo inataka kuona wanafunzi wote wanaotakiwa kwenda Sekondari wanakwenda shule, hivyo ni vema wananchi wakishikamana na serikali ili kuona namna ya kuweza kumaliza changamoto za shule.

Katika hatua nyingine Mjema alizungumzia suala la usafi katika wilaya yake, ambapo alisema manispaa hiyo imepiga hatua katika suala hilo na kuongeza kuwa wanacho kifanya sasa ni kuhakikisha wanaongeza vifaa zaidi vya kufanyia usafi na sehemu zakutupa taka .

Alisema hapo awali walikuwa na uwezo wa kukusanya uchafu zaidi ya tani 300 kwa siku, lakini hivi sasa wanakusanya tani 400 kwa siku na sikuchache zijazo watakusanya zaidi ya tani 1000 na watajipanga kuona kwamba uchafu huo unazalishwa kitu kingine mbadala.


No comments:

Post a Comment