28 January 2013

Waislam watakiwa kujiepusha na vurugu



Na Florah Temba,Moshi.

WAISLAM kote nchini,wametakiwa kujiepusha na vurugu mbalimbali ambazo zinahatarisha amani na utulivu wa nchi, kutokana na kwamba madhara ya uvunjifu wa amani katika Taifa lolote duniani ni makubwa.


Wito huo ulitolewa jana mjini Moshi kwenye sherehe za maulidi na mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya sherehe hizo mkoani Kilimanjaro Bw. Ibrahimu
Shao ambapo alisema Uislam ni amani na si vurugu.

Bw.Shayo alisema waislamu katika kumuenzi Mtume Muhamadi hawana budi kufuata vitendo vyake ikiwa ni pamoja na kuimarisha amani na utulivu katika
Taifa.

“Ndugu zangu waislamu, tujiepushe na vurugu zinazohatarisha amani na utulivu ndani ya Taifa letu,kwani uislamu ni amani na mtume wetu Muhammad
alikuwa ni mtu wa amani kama uislamu unavyojieleza na kwa hakika ninyi nyote mnafahamu madhara ya Taifa lisilokuwa na amani,”alisema Bw. Shayo.

Katika hatua nyingine, Bw. Shayo aliwataka waislamu kuunga mkono miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa na serikali ili kuhakikisha
inafanikiwa na kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Akizungumza katibu wa baraza la Kiislamu Mkoani Kilimanjaro Bw. Rashid Malya, alisisitiza waislamu kudumisha amani na utulivu katika nchi na kusema kuwa watu wanaofanya vurugu kwenye nyumba za ibada wana akili ndogo hivyo wanapaswa kukemewa.

Alisema ni vema waislamu wote wakaungana kupinga vitendo vya uvunjifu wa amani vitakavyojitokeza na kuhakikisha wale wenye nia mbaya ya kutaka
kuvuruga amani hiyo wanachukuliwa hatua mara moja.

“Wanaofanya urugu kwenye nyumba za ibada wana akili ndogo sana,na huu ni ushabiki usio na tija,tuwahimize watanzania, tuache vurugu, “alisema.

Katika sherehe hizo ambazo kimkoa zimefanyika viwanja vya msikiti wa Riadha mjini Moshi, zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini hiyo
kutoka katika wilaya zote saba za mkoa huu na mkuu wa wilaya ya Moshi, Dkt.Ibrahim Msangi ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.

Katika kusheherekea siku hiyo waislamu mkoani Kilimanjaro waliweza kula chakula na watoto wa mazingira magumu na yatima wanaolelewa katika vituo
mbalimbali mjini Moshi,wazee pamoja na wagonjwa katika hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi.




No comments:

Post a Comment