28 January 2013

Kiwanda cha kutengeneza mafuta ya albino kuzinduliwa MoshiRachel Balama na Anneth Kagenda

KIWANDA cha kutengeneza mafuta kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kilichopo mkoani Moshi kilichogharimu sh. milioni 68 kinatarajiwa kuzinduliwa wakati wowote kuanzia sasa.


Akizungumza na waandishi wa Habari Dar es salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la Under the Same Sun (UTSS), Peter Ash, alisema kuwa mafuta hayo yatatengenezwa hapa nchini na kusambazwa bure na shirika hilo kwa muda wa miezi 12, ambapo muhusika anauwezo wa kutumia kopo moja kwa miezi sita.

Alisema kuwa gharama ya jengo la kiwanda hicho zimetolewa na Mkurugenzi wa Mfuko wa Kamana,Paul Ash  ambapo fedha za uendeshaji pamoja na gharama zingine zitatolewa na shirika hilo kwa kipindi cha miezi 18.

Alisema kiwanda hicho ambacho ni cha kwanza kufunguliwa nchini Tanzania kinachotengeneza mafuta yajulikanayo kama'kilimanjaro SunCare' ni kwa ajili ya watoto na watu wazima na yatasaidia kuimarisha ngozi zao pale wanapopigwa na jua pamoja na kuwasaidia wasipate kansa hivyo kuendelea kuishi maisha marefu.

Katika hatua nyingine, Ash, ameipongeza Halmashauri ya Magu Mkoani Mwanza kwa kuanzisha kliniki maalum kwa ajili ya matibabu bure kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.

Alisema kuwa huduma zinapowafikia watu pale walipo itasaidia hiku akiitaka serikali na taasisi nyingine kuiga mfano wa halmashauri ya Magu ambayo kwa muda mrefu imeonekana kuwa ni kitovu cha ushirikina.

"Inatia moyo kwa wilaya hiyo kuanzisha kliniki maalum ya albino kwa kuwa  imani nyingi za kishirikina zimejikita katika wilaya hiyo ikilinganishwa na wilaya nyingine zilizopo mkoani humo," alisema.

Alisema watu 71 wameuawa ambapo katika kesi watano wamehukumiwa kunyongwa, kesi zipo nane, 24 majeruhi na 19 wamefukuliwa huku wengine wakinyofolewa viungo.

Alisema pia kutokana na ukatili huo inaonesha kwa silimia 95 watu wenye ulemavu wameuawa na makaburi yao kufukuliwa huku kesi zikiwa hazijatajwa wala kufika mahakamani.

Aidha alisema kuwa haki bado haijatendeka kwa watu hao na kuitaka serikali iwatendee haki watu hao kwa kuhakikisha kuwa kesi zote zinazohusu ukatili dhidi yao zinasikilizwa na kutolewa hukumu.

No comments:

Post a Comment