15 January 2013

Wahamiaji 21 wakamatwa Kilimanjaro



Na Florah Temba, Moshi

JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro, linawashikilia wahamiaji haramu 21 kutoka nchini Ethiopia kwa tuhuma za kuingia
nchini kinyume cha sheria.


Kamanda wa Polisi mkoani humo, Robert Boaz, alithibitisha kukamatwa kwa wahamiaji hao na kusema kuwa, biashara hiyo
inafanywa na mtandao unahusika kuwasafirisha.

“Hawa wahamiaji waliingia nchini kwa njia za panya, bila ya
kuwa na vibali...walikamatwa Januari 12 mwaka huu, saa 7:30
usiku katika eneo la Same Mjini, mkoani hapa,” alisema.

Aliongeza kuwa, wahamiaji hao walikamatwa na askari waliokuwa doria wakiwa kwenye gari lenye nambari za usajili T 773 ALA, aina ya  Toyota Land Cruiser, iliyokuwa ikiendeshwa na Bw. John Malamla (28).

Alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na idara ya uhamiaji mkoani humo, wanaendelea na chunguzi ili kuubaini mtandao ambao unahusika kufanya biashara hiyo.

Hata hivyo, Kamanda Boaz hakusema wahamiaji hao waliingia nchini lini na walikuwa wakienda wapi ila alifafanua kuwa, taratibu za kisheria zinaendelea ili waweze kufikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment