15 January 2013

Afa kwa kuangukiwa na kifusi mgodini


Na Suleiman Abeid, Shinyanga

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti yaliyotokea mkoani Shinyanga, likiwemo la msimamizi wa machimbo ya madini ya dhahabu, Wilson Mapengo (28), kuangukiwa na kifusi cha udongo akiwa katika shughuli za kukagua mashimo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Evarist Mangalla, alisema marehemu ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyankende, wilayani Kahama, alifariki juzi saa 12 jioni.

Alisema tukio hilo limetokea katika machimbo madogo ya dhahabu yaliyoko Kijiji cha Mwabomba, wilayani Kahama wakati marehemu akiendelea na kazi ya ukaguzi katika moja ya mashimo ghafla kifusi cha udongo kilikatika, kumfukia na kufa papo hapo.

Katika tukio jingine, mkazi wa Kijiji cha Kizungu, aliyefahamika kwa jina moja la Lucas (33), ameshambuliwa na wanakijiji wenye hasira baada ya kukwama kufanya jaribio lake la unyang’anyi juzi saa 5:30 usiku, katika Kijiji cha Lyabukande, wilayani Shinyanga.

Aliongeza kuwa, siku hiyo ya tukio marehemu alivamia nyumba ya Bi. Mary Bunzali kwa nia ya kutaka kupora mali lakini mwanamke huyo alifanikiwa kumdhibiti na kupiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa wanakijiji wenzake.

Alisema baada ya wanakijiji kufika katika eneo hilo, walianza kumshambulia kwa fimbo, mawe na marungu sehemu mbalimbali
za mwili wake hadi kufa, maiti yake kuchomwa moto na kuteketea.

Hata hivyo, Kamanda Mangalla alisema hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi. Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

No comments:

Post a Comment