03 January 2013
'Waganga wa tiba asili acheni udanganyifu'
Na Anneth Kagenda
WAGANGA wa tiba asili nchini, wameshauri kufanya kazi zao kwa kufuata masharti yanayowekwa na Serikali yakiwemo kupata vibali halali vya kufanya shughuli hizo ili kupunguza udanganyifu kwa wananchi kuwa, kutoa kafara ya kuua kunasaidia kupata utajiri.
Ushauri huo umetolewa Dar es Salaam juzi na mmoja wa waganga kutoka Mkuranga Dkt. Kassim Mswahili, wakati akizungumza na gazeti hili juu ya udanganyifu unaofanywa na baadhi ya waganga wasio na kibali cha kutoa tiba kwa wananchi.
Alisema waganga wengi ambao wamekuwa wakifanya shughuli
hizo, hawana vibali vya Serikali na wamekuwa wakiwadanganya wananchi kuwa, kafara ya kuua itawasaidia kupata ajira.
“Nawaomba wananchi msidanganywe na kauli hizi, baadhi ya waganga wamekuwa wakiwaambia mkiua katika shughuli zenu za uchimbaji madini au uvuvi mtafanikiwa sana, wanaosema hivyo ni waganga feki na hawaijui kazi hii,” alisema Dkt. Mswahili.
Aliongeza kuwa, lengo la kutoa ushauri huo kwa wananchi ni kutaka wabadilike na kuwapuuza waganga wa aina hiyo. “Naiomba Serikali
ilitilie mkazo suala la watu wanaotoa tiba hizi kuwa na vibali ili jamii kubwa isiendelee kupotoshwa,” alisema.
Dkt. Mswahili aliwashauri watoa tiba wenzake kuwa, umefika wakati wa kujiunga katika chama cha waganga nchini ili iwe rahisi kupata kibali kwa Mganga Mkuu wa Wilaya au Manispaa na kuacha kufanya kazi bila ya kutambulika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment