28 January 2013

Vodacom yataka klabu kutoa ushindani


Na Zahoro Mlanzi

WADHAMINI wa Ligi Kuu Bara, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom imezitaka klabu zinazoshiriki ligi hiyo kuendelea kuonesha ushindani, kama zilivyofanya katika mzunguko wa kwanza.

Ligi hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho katika nyasi za viwanja sita tofauti, ikiwa ni mzunguko wa lala salama.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa Nje wa kampuni hiyo, Salim Mwalimu alisema wamefurahishwa na kiwango kilichooneshwa katika mzunguko wa kwanza na hii inaonesha soka nchini linapiga hatua.

"Kama wadhamini tunaona fahari timu zikicheza kwa ushindani kwa maana mpira unachezwa zaidi uwanjani, kuliko nje ya uwanja tofauti na ilivyokuwa zamani," alisema Mwalimu na kuongeza;

"Mashabiki, wachezaji wameonesha taswira jinsi soka linavyokwenda, kwani unaona wazi jinsi wanavyoshagilia na wachezaji wanavyojituma uwanjani, tunaomba waendelee na ushindani huo hata kwa mzunguko wa pili." alisema.

Alisema katika kuonesha ligi imekuwa na ushindani mkubwa, hata zile zinazojiita timu kubwa zimekuwa zikipata matokeo tofauti, hususani katika mechi za mikoani na kujikuta zikiumiza vichwa kwa kila mechi.

Mwalimu alisema hata katika usajili inaonekana jinsi timu zinavyogombania wachezaji na hiyo inatokana na ugumu wa ligi na ndiyo maana, kila timu inataka kuimarisha kikosi chake ili ifanye vizuri zaidi ya mzunguko uliopita.

Alisema kampuni yake itaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Ligi, pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kalba mwezi ujao haujaisha kwani mambo mazuri yatakuja hivyo klabu zikae chonjo.

Pia alimpongeza Rais wa TFF, Leodegar Tenga kwa kuliongoza shirikisho hilo kwa miaka nane akiwa na mafanikio makubwa na kumuomba aendelee kutoa mchango wake katika kuendeleza soka la Tanzania.

Naye Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura akizungumzia maandalizi ya ligi hiyo, alisema kila kitu kimekamilika ambapo Kamati ya Waamuzi, tayari imeshawapanga waamuzi wake pamoja na makamishna.

Alisema kikubwa anawaomba mashabiki wa timu hizo kushangilia kwa nidhamu, bila kuvunja sheria kwani kwa kufanya hivyo, wataziweka timu zao katika wakati mgumu kutokana na adhabu zitakazotolewa.

No comments:

Post a Comment