28 January 2013

Kocha wa kikapu akata tamaaNa Amina Athumani

KOCHA wa timu ya Taifa ya mpira wa kikapu, Evarist Mapunda amesema matumaini ya Tanzania kuingia hatua ya robo fainali ni madogo.


Mapunda aliyasema hayo Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na gaazeti hili kuhusiana na hatma ya Tanzania kuingia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo huku dalili za kubakiza kombe la michuano hiyo nyumbani zikiwa tayari zimeota mbawa.

Mapunda alisema timu za Tanzania ya wanaume na wanawake mpaka jana hazikufanikiwa kushinda hata mechi moja tangu kufunguliwa kwa michuano hiyo Januari 21 mwaka huu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda,

"Kilichobaki sasa kwa timu zetu ni kujifunza kupitia kwa timu nyingine maana sisi hatukushiriki mashindano haya kwa muda mrefu tofauti na wenzetu,"alisema Mapunda.

Alisema Kichapo mfululizo kwa timu za Tanzania wao kama benchi la Ufundi hawahusishi na chochote kile ikiwemo kinachozungumziwa kuwa kinatokana na kutolipwa posho kwa wachezaji hao.

"Mimi naamini benchi la ufundi tunafanya kazi yetu na hata uongozi unafanya kazi yao hivyo sitaki kujishirikisha na ishu yoyote kama ni matatizo yaliyopo ni madogo ambayo hayahusiana na kufungwa kwetu,"alisema Mapunda.

"Pia tatizo la sisi watanzania tunapenda sana kukata tamaa mapema pia watu wakumbuke kwamba huwezi kumkamua ng'ombe maziwa pasipo kumpa majani unafikiri matokeo yake yangekuwa nini?,"alihoji Mapunda.

Alisema hata hivyo hatma ya timu ya wanawake ni mechi mbili zilizobaki kati yao na Uganda iliyotarajiwa kucheza jana jioni na nyingine watakayochuana leo na Burundi.

Kwa upande wa wanaume jana hawakuwa na mechi hivyo watajitupa uwanjani leo kujaribu tena bahati yao.

Timu za Tanzania zilianza kwa kusuasua baada ya mechi za kwanza za ufunguzi kufungwa huku wanawake wakicharazwa na Kenya kwa pointi 74-32, wakafungwa na Rwanda 95-52 kisha wakatandikwa na Misri 100-26.

Kwa upande wa wanaume walipoteza mechi ya ufunguzi kwa kufungwa na Uganda na ikapoteza mechi yake dhidi ya Misri na ikacharazwa na Rwanda.

Mpaka sasa katika msimamo wa michuano hiyo timu za Misri ambao ni mabingwa mara nyingi wa michuano ya kanda ya tano na Rwanda ambao ni mabingwa watetezi ndio wanaoongoza michuano hiyo kwa timu za wanaume kwa kutofungwa mchezo hata mmoja tangu kuanza kwa michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment