18 January 2013

Uhamiaji yakamata wahamiaji 234Na Wilhelm Mulinda, Mwanza

IDARA ya Uhamiaji, mkoani Mwanza, imewakamata wahamiaji haramu 234 kwa nyakati tofauti mwaka 2012 wengi wao wakiwa
raia wa nchi ya Congo (DRC), pamoja na Burundi.


Akizungumza na Majira jana, Kaimu Ofisa Uhamiaji mkoani humo, Bi. Anna Yondan, alisema idadi hiyo imeshuka kutoka wahamiaji 336 waliokamatwa mkoani humo mwaka 2011 ambao ni raia wa
Congo, Burundi na Ethiopia.

Alisema sababu za kupungua idadi ya wahamiaji mwaka 2012 ni kutokana na elimu waliyotoa kwa wananchi katika Wilaya zote mkoani humo kuhusu namna ya kuwatambua wahamiaji haramu pamoja na madhara wanayoweza kusababisha kwa jamii.

“Mbali ya elimu hii kuitoa kwa wananchi pia iliwafikia Maofisa Watendaji wa kata na mitaa katika Wilaya zote, hatua hii imesaidia kuwabaini wahamiaji na kutoa taarifa,” alisema.

Aliongeza kuwa, ili kupambana na uhamiaji haramu idara hiyo imeweka Maofisa Uhamiaji katika kata zote za Wilaya ya Ilemela pamoja na Nyamagana ambazo zinamwingiliano mkubwa wa watu.

Aliwaomba wananchi kushirikiana na idara kwa kutoa taarifa za watu wasiowafahamu ili waweze kuchunguzwa.

No comments:

Post a Comment