29 January 2013

Uchumi umekua kwa asilimia 6.7-Mgimwa

Na Eliasa Ally, Iringa

WAZIRI wa Fedha na Uchumi Dkt.william Mgimwa ambaye ni mbunge wa jimbo la Kalenga katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa Vijijini amesema kuwa hali ya uchumi hapa nchini inaendelea kuimarika ambapo kwa sasa uchumi ndani ya nchi umekua hadi kufikia asilimia 6.8 hali ambayo inaleta matumaini makubwa kwa wananchi na serikali yao.


Hayo aliyasema jana alipokuwa akizungumza na wananchi katika uwanja wa Mwembetogwa wakati Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa Philipo Mangula alipokuwa amekuja mkoani Iringa na kuzungumza na wananchi wa mkoa wa Iringa ambapo alisema kuwa kuna ongezeko kubwa linaloonesha uchumi wa nchi kwa sasa unakua kwa kasi tofauti na hapo awali ambapo uchumi ulikuwa unalalamikiwa.

Dkt.Mgimwa alisema kuwa serikali ya CCM inaendelea kuhakikisha kuwa uchumi ndani ya nchi unaendelea kukua kwa kasi na kuwawezesha wananchi pamoja na serikali yao kupata maendeleo sitahiki katika kufanya biashara, kuuza mazao na kwa upande wa serikali kuhakikisha wanakusanya kodi kufikia malengo ambayo yamewewekwa na serikali inayosimamiwa na CCM.

"Kwa sasa maendeleo yanapiga hatua kubwa kiuchumi, takwimu za sasa zinaonesha kuwa uchumi wetu ndani ya nchi umekua kwa asilimia 6.8, hii ni hatua kubwa sasa hivyo katika kila hatua ambayo tunapiga tutahakikisha tunawarifu ninyi wananchi ili mweze kufahamu bayana hali yetu ya kukua kwa uchumi wa ndani", alisema Dkt. Mgimwa.

Aidha, alisema kuwa kutokana na uchumi wa ndani ya nchi kuendelea kuimarika na kukua kwa kasi, wafanyabiashara, wakulima na wajasiliamali wataendelea kukuza mitaji yao ambapo aliwataka kila mwananchi aendelee kuhakikisha kuwa anajiajiri na siyo anakaa
vijiweni na kutaka serikali ndiyo imletee maisha bora huku akiwa amekaa na hawataki kufanya kazi ambazo zitawaingizia vipato.

Aliongeza kuwa maisha bora kwa wananchi yanakuja baada ya wao wenyewe
kujishughulisha, kufanya kazi, kuzalisha shughuli za kiuchumi na kuhakikisha kuwa katika mitaji yao waliyonayo wanendelea kukuza vipato na kushirikiana na serikali katika kufanya kazi za kuajiriwa na kujiajiri mtu binafsi hususani katika shughuli za ujasiliamali.

No comments:

Post a Comment