28 January 2013

TBS yajipanga kumaliza tatizo la bidhaa bandia nchini



Na Mwandishi Wetu

PAMOJA na chagamoto mbalimbali zinazolikabili Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limeweza kutimiza wajibu wake wa kuwahudumia Watanzania na wateja wake kwa ujumla na kuahidi kutoa huduma bora mwaka huu.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Leandri Kinabo, anasema shirika lake limepania kutoa huduma bora mwaka huu.

Anazitaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni uhaba wa vitendea kazi, hasa ikizingatiwa vitendea kazi vya maabara zao hununuliwa kwa bei aghali, upungufu wa rasilimali watu, uhaba wa fedha za maendeleo na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu viwango.

“Pamoja na  changamoto hizo zilizojitokeza mwaka jana, TBS imeendelea kutekeleza majukumu yake mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa viwango,kudhiti bidhaa duni, kutoa huduma za upimaji na ugezi pamoja na kutoa mafunzo kwa wenye viwanda, wajasiriamali na watoa huduma,” anasema.

Anasema hadi mwishoni mwa mwaka jana shirika limeweza kuandaa viwango zaidi ya 100 na kwa kutumia wataalam wake na wadau mbalimbali wa ndani na nje shirika lina kamati za kitaalam zaidi ya 100.

Anasema, baadhi ya viwango vilivyondaliwa kuwianishwa ni pamoja na sabuni za unga, mabati, nyaya za umeme, kondomu za kike na matandiko ya hospitali.

Nyingine ni viwango vya dizeli na petrol ambavyo viliwianishwa katika nchi za Afrika Mashariki wakati kwa upande wa bidhaa za vyakula, viwango mbalimbali viliandaliwa  vikiwemo nafaka kama mahindi, viungo, vinywaji mbalimbali visivyo na kileo na viwango na kanuni mbalimbali za za upimaji.

Kinabo anafafanua kwamba juhudi za kuwianisha viwango vya Afrika Mashariki ziliendelea vizuri kwa mwaka jana kwa kushirikiana na nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.

“Pia tulifanya mkutano wa nchi za SADC ili kuwianisha viwango vya biashara ma kwa sasa Tanzania ndiyo Mwenyekiti wa kamati ya Viwango kwa nchi za SADC,".

“Itakumbukwa kuwa kwa mwaka huu nchi yetu ilikuwa ni mwenyeji wa mkutano wa Mashirika ya Viwango Afrika (ARSO) ambao ulifanyika Aruisha, mkutano huu ulikuwa na umuhimu  wa pekee kwani uliandaa katiba mpya ya mashirika ya viwango Afrika," anasema.

“Kwa kweli tumejitahidi kadri ya uwezo wetu kuandaa mikutano hiyo na ilifanyika katika hali ya ufanisi,” anafafanua.

Anawashukuru wataalam mbalimbali wadau wanaofanya kazi pamoja na TBS kutoka sekta mbalimbali kwa kulifanya shirika kuandaa viwango vya kitaifa hadi sasa zaidi ya 1500.

Kwa upande wa udhibiti ubora anasema kwamba kwa mwaka jana shirika lake liliendelea kutoa huduma hiyo kwa kwa viwanda vya ndani na nje ya nchi.

“Kuhusu udhibiti wa ndani shirika limeendelea kuhudumia viwanda na limetoa leseni mpya 85 za kutumia alama ya ubora na vyeti 15 vya ubora”.

Anasema kwamba shirika lake kwa mwaka jana liliendelea na utaratibu wake wa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali kwa lengo la kuwawezesha kuzalisha bidhaa bora.

Anasema kwamba mwaka jana jumla ya wajasiriamali 20 walipewa alama ya ubora na kufikisha idadi ya wajasiriamali 226 ambao wamepatiwa alama ya ubora ya TBS katika bidhaa wanazozalisha.

“Ikumbukwe kwamba hakuna viwango pekee kwa ajili ya wajasiriamali bali nao huzalisha bidhaa katika ubora unaokubalika,”

Anabainisha kwamba kwa mwaka 2012, shirika lilitoa mafunzo ya uzalishaji bora kwa wajasiriliamali wa mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Tanga Kilimanjaro na Arusha na kwamba bidhaa zao zilizopewa alama ya ubora ya TBS ni pamoja na Mvinyo, Mafuta ya alizeti, asali, maji ya kunywa, sabuni na jam.

Kwa upande wa udhibiti wa bidhaa za nje ya nchi, anasema shirika lilianza utekelezaji wa mfumo wa upimaji ubora wa bidhaa kabla ya kuingizwa nchini yaani PVoC kuanzia Februali mwaka jana na kwamba kazi hiyo hufanywa duniani kote na mawakala walioteuliwa kwa njia ya zabuni.

“Katika jitihada zetu za kusogeza huduma karibu na wananchi, shirika lilifuugua ofisi katikati ya Jiji Mtaa wa Samora ambako ni karibu na bandari na ofisi za forodha,” anasema.

Kinabo anasema hivi karibuni, TBS imeanzisha kitengo maalum cha kupima mafuta ndani ya maabara ya kemia baada ya kupata vifaa vya kisasa vya kupimia bidhaa hizo.

Mwishoni mwa mwaka jana shirikisho la Wenye viwanda nchini (CTI) lililipongeza TBS  kwa kuwahudumia vizuri wenye viwanda nchini na pia katika ushirikiano ambao TBS inautoa katika vita dhidi ya bidhaa hafifu na bandia zinazoingizwa nchini.

Mwenyekiti wa CTI, Felix Mosha anasema kwamba TBS imekuwa ikijitahidi kukabiliana na uingizaji holela wa bidhaa hafifu na bandia nchini hususan kwa kuzingatia ukaguzi wa bidhaa hizo wakati wa uingizwaji wake  katika soko la ndani ya nchi.

Katika mkutano Mkuu wa 20 wa CTI wa mwaka uliohusu umuhimu wa udhibiti wa uuzaji wa bidhaa zinazokidhi viwango, Mosha anasema kwamba taasisi yake imekuwa ikishirikiana vema na TBS katika kuhakikisha kwamba bidhaa zinazoingizwa nchini zinakuwa kwenye ubora wa viwango unaokubalika.

Mosha anaitaja TBS kuwa miongini mwa taasisi za umma ambayo imekuwa ikitoa ushirikiano wa haraka katika kwa  wanachama wa CTI.

Anaishukuru serikali kwa kuanzisha ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuingia nchini katika jitihada za kuzipunguza au kuziondoa kabisa sokoni bidhaa hafifu.

Katika utafiti uliofanywa hivi karibuni kuhusiana na “Mapitio ya sheria na taratibu kuhusiana bidhaa bandia au hafifu, imebainika kwamba soko letu lina asilimia 20 ya bidhaa za aina hiyo zinazoingizwa nchini.

“Madhara ya bidhaa za aina hiyo ni makubwa katika uchumi wetu, na kwamba ni bidhaa za aina hiyo zinapunguza mahitaji ya bidhaa zenye ubora wa viwango zinazozalishwa na viwanda vya ndani kutokana na ukweli kwamba bidhaa bandia na hafifu zinauzwa kwa bei ya chini sana,” anasema.

Anasema madhara ya soko kuwa na bidhaa bandia na hafifu kuwa ni mengi lakini moja wapo ni kuwakatisha tamaa wawekezaji wanaotaka kuwekeza hapa nchini katika viwanda vya uzalishaji wa bidhaa za vifaa vya umeme, mashine za aina mbalimbali na bidhaa za kemikali.

“Mbali na hayo serikali pia inapoteza mapato kutokana na uingizwaji nchini wa bidhaa zenye thamani ndogo ambazo ni bandia au hafifu,” anafafanua.

Anasema kwamba bidhaa za aina hiyo pia zinahatarisha usalama wa watumiaji kwa kuwa hazina viambata au malighafi za kutosha katika kutengeneza bidhaa husika kwa matumizi ya wateja.

Pamoja na kuipongeza serikali kwa kuanzisha ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuingia sokoni, jitihada zaidi zinabidi kufanywa na serikali katika kuhakikisha kwamba makampuni yanayopewa kazi za ukaguzi na TBS katika nchi bidhaa zinakotoka yanafanya kazi zao kwa uadililifu ili kuhakikisha kwamba ni bidhaa halisi pekee ndizo zinazoingia nchini.

“Tunapenda kuihakikishia serikali na TBS kwa ujumla kwamba Shirikisho la Wenye Viwanda nchini litafanya kila liwezalo ili kuhakikisha kwamba bidhaa bandia na hafifu zinapotea kabisa sokoni,” anasema.

Anabainisha kwamba shirikisho liko kwenye mchakato wa  kuuelimisha umma njia za utambuzi wa bidhaa bandia na hafifu na kuwaelewesha watumiaji juu ya madhara ya matumizi ya bidhaa za aina hiyo kwa nchi, afya na usalama wao.

Anasema wazo la kuanzisha elimu ya aina hiyo kwa umma linatokana na tafiti walizofanya kuhusiana na bidhaa za aina hiyo.

“Tunaiomba Wizara na wadau wengine watuunge mkono katika jitihada hizo na kwamba ni imani yetu kwamba ushindi dhidi ya vita ya bidhaa hizo unategemea kwa kiasi kikubwa uelewa wa watumiaji juu ya madhara ya bidhaa hizo kwa ujumla wake,” anasema.

Kuhusu mazingira ya sekta ya viwanda hapa nchini, Mosha anasema kwamba mbali na athari za uagizaji wa bidhaa hafifu, sekta ya viwanda inaathiriwa na mambo mbalimbali ikiwamo gharama kubwa za ufanyaji wa biashara hapa nchini mfano gharama kubwa za nishati ya umeme, kukatika katika kwa nishati hiyo na mgowo wa umeme wa kila mara.

“Pamoja na haya pia wingi wa aina mbalimbali za kodi wanaotozwa wenye viwanda ni sababu nyingine inayozifanya bidhaa za Tanzania zisishindane kwa usawa na bidhaa kutoka nchi nyingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki pamoja na zile za nchi za SADC,” anasema.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt.Abdallah Kigoda, anasema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na viwanda vingi vya kiwango cha kati ambavyo vitasaidia kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

Anasema kwamba serikali inafanya jitihada kubwa ili kuhakikisha kwamba sekta ya viwanda inakua kwa kiwango cha kuridhisha na anazitaja jitihaza hizo kuwa ni pamoja na kuanzisha ukanda maalum wa kiuchumi wenye vivutio vya aina mbalimbali na kwamba jitihada hizo zimezaa matunda baada ya wawekezaji wengi kujitokeza.

Kuhusu sekta ya nishati ya umeme, Waziri anasema kwamba serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, itahakikisha kwamba kwamba tatizo la nishati ya umeme linakwisha ifikapo mwaka 2015 kwani nchi itaweza kuzalisha Megawati 2300 badala ya 1300 za sasa.

“Ni imani yangu kwamba kiwango hicho kitakidhi mahitaji ya sekta ya viwanda na ya watumiaji wengine wakiwamo wa majumbani “ anasema.

Anasema kuwa wakati serikali ikiwa imedhamiria kuliondoa tatizo la bidhaa hafifu sokoni, ni dhahiri ushirikiano wa wazalisaji, wafanyabiashara na wa walaji ni muhimu katika kufanikisha vita dhidi ya bidhaa hizo.

Kinabo anasema dhima ya Shirika la Viwango Tanzania ni kueneza uelewa na kukuza matumizi ya viwango na kanuni za udhibiti wa ubora katika sekta za viwanda na biashara, kwa nia ya kuunga mkono juhudi za kitaifa za kuzalisha bidhaa na huduma bora zenye uwezo wa kushindana katika masoko ya ndani na nje, lengo likiwa ni kukuza uwepo wa bidhaa na huduma bora na salama kwa umma wa Watanzania na kuchochea maendeleo ya Taifa kiuchumi.

Anasema Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kwa kuzingatia dhamana liliyopewa, linahakikisha linatoa huduma bora, ambazo ni pamoja na utayarishaji wa viwango na uhakiki wa ubora, kwa kukidhi na hata kuvuka matakwa ya wateja, ili kudumisha imani yao.


No comments:

Post a Comment