28 January 2013

Tusitafute Katiba Mpya Pekee



NENO “Pekee” kwa tafsiri ya lugha ya kigeni yaweza kuwa “Special”.  Kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita tumeweza kutawaliwa na katiba yenye sifa za kipekee, nasema katiba ya kipekee kwa vile katiba tunayoitumia hivi sasa ilikuwa haifanani na katiba nyingine yoyote ile duniani.


Katiba ambayo mtu mmoja anafanya kila kitu, ana wasaidizi wengi wa kumsaidia kufanya kazi na kuamua lakini hawaruhusiwi kufanya hivyo. Upekee ni mzuri kama upekee huo ungekuwa umelenga maslahi ya umma, lakini upekee unapolenga maslahi ya wachache si upekee mzuri kwa jamii yoyote ile inapenda amani duniani.

Sasa hivi tupo katika mchakato wa kutafuta katiba mpya, lakini bado haijajulikana kama tunatafuta katiba ya kipekee kama iliyopo hivi sasa au tunatafuta katiba inayofanana na katiba za nchi zingine? Kulingana na baadhi ya maoni yanayotolewa na viongozi wa umma waliopo madarakani na wale waliostaafu inaonekana wao wamefurahishwa sana na matokeo mazuri ya katiba iliyopita hivyo wangependelea watuandikie tena katiba mpya ya kipekee kama iliyopo hivi sasa!

Katiba ndiyo inayopima maendeleo ya jamii yoyote ile duniani, ukisoma katiba ya nchi yoyote bila ya kujali kwamba ni Ulaya, Afrika, Amerika au Asia unaweza kujua kiwango cha maendeleo ya nchi hiyo hata kama hujawahi kufika huko.

Katiba ni mwongozo wa jamii ambao unaonyesha ni jinsi gani watu wanagawana majukumu katika shunguli za umma za kila siku, na kuhakikisha kwamba zinatekelezeka na jamii inanufaika na shughuli hizo. 

Watawala wanaona katiba pekee ya Nyerere imetusaidia kutujengea amani na utulivu, ikiwa ni pamoja kuleta maendeleo makubwa katika jamii na kukuza kiwango cha elimu na teknolojia ya kizazi cha kisasa, kupunguza kiwango cha umaskini, kukua kwa kilimo cha kisasa, kupanuka kwa miundombinu, kupungua kwa vitendo vya kutoa na kupokea rushwa na ufisadi.

Kwa mafanikio haya Tanzania iliyoyapata kutokana na katiba ya Nyerere watawala wetu wameonelea waandike katiba mpya yenye upekee wa ziada ikizingatia kutokumpunguzia rais madaraka na kujaribu kumuongezea madaraka makubwa zaidi ili aendelee kuyaboresha haya yote niliyoyataja hapo juu kwa manufaa ya umma wa Watanzania!

Nchi nyingi duniani zinapoandika katiba mpya huwa hawajifungii chumbani na kuanza kuandika katiba pekee, hapana, bali wanatafuta ushauri toka nchi mbali mbali zilizoendelea ikiwa ni pamoja na kutafuta katiba za nchi hizo kupitia kwenye balozi za nchi hizo zilizopo kwenye nchi husika.

Huwezi kujifungia chumbani ujidanganye kwamba unaandika katiba ya kipekee kwa ajili umma wa Watanzania, ukifanya hivyo utakuwa unaugandamiza umma, kwa vile katiba ni Teknolojia na 'Know – How' ya hali ya juu hivyo ukijifanya hutaki kutumia reference za watangulizi ambao waliwahi kuandika katiba utakuwa unajidanganya na wale wote unaowaandikia katiba hiyo!

Ukikuta Mwanazuoni anaandika “Article” au “Paper” au “Kitabu” bila ya kutumia 'reference' za wanazuoni wengine waliotangulia ambao waliwahi kuandika kitu kinachofanana na chake, basi lazima ujue kwamba hayupo makini.

Ni mwanazuoni mbabaishaji, na kama ukimchunguza kiundani utakuta alipita njia za uwani au vichochoroni!

Mimi naamini kama kiongozi amechaguliwa na umma kwa kura za ukweli na siyo kura za kuchakachuliwa, basi kiongozi huyo hawezi kuandika katiba inayouhujumu umma. Hawezi kufanya hivyo kabisa kwa vile yupo pale kwa ajili ya umma, na kwa vile yupo kwa ajili ya umma ni lazima umma utakuwa unaona wazi wazi kwamba huyu yupo hapa kwa ajili yetu zaidi kuliko kwa ajili yake binafsi, lakini ukikuta kiongozi anaubana umma kwa manufaa yake binafsi ni lazima ujue kwamba kiongozi huyo alipita njia za vichochoroni kupata nafasi hiyo.

Nchi za Kusini mwa Asia (Malaysia, South Korea, Taiwan, Hong Kong, Indonesia, Singapore na Thailand) kwa jina mashuhuri “The Tigers” miaka ya mwanzoni mwa sitini zilikuwa nyuma kimaendeleo na Teknolojia kwa Tanzania, nchi hizi ziliona umuhimu wa katiba kama mwongozo wa jamii zao, hivyo bila kusita na bila ubinafsi ziliandika katiba nzuri zenye manufaa kwa umma.

Hawakujifungia chumbani na kuandika katiba zenye sura za kipekee kama ile aliyotuandikia Nyerere, hapana, wao waliandika katiba za nchi zao lakini walichukuwa mambo mengi sana katika katiba za nchi kama vile, Marekani, Japan, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.

Ndiyo maana kwa kipindi cha muda mfupi cha miaka 50, nchi hizi zimetoka dunia ya tatu na kujiunga na dunia ya kwanza! Dunia nzima inazishangaa nchi hizi, na nchi hizi zinaeleweka kama nchi zenye miujiza ya uchumi duniani (economical miracles)!

Katiba ya Afrika ya Kusini ni moja kati ya katiba nzuri sana duniani, licha ya kwamba katiba hiyo iliandikwa na watu wawili tu, kwa kipindi kisichozidi siku 90.

Pamoja na kuwa katiba nzuri sana duniani, lakini hawakujifungia chumbani na kuandika katiba ya nchi yao, bali walichukua mambo mengi kwenye katiba hizo.

Marekani pamoja na kwamba ni taifa kubwa duniani kwa kila kitu muhimu, lakini walipokuwa wanaandika katiba ya nchi yao, hawakujifungia chumbani na kuanza kuandika katiba pekee ya Kimarekani, hapana, bali walitafuta ushauri na uzoefu toka kwenye katiba za nchi za Ulaya, na kuweza kupata katiba nzuri ambayo imelifanya taifa hilo kuwa kubwa kiuchumi na kisayansi na teknolojia duniani.
 
Kwa muda wa miaka 52 sasa tumeweza kujifungia kama kisiwa na kuweza kujenga jamii yenye woga isiyojiamini na wala isiyoweza kuthubutu kudai hata mambo ya msingi ya maisha yao! Kulingana na mafanikio hayo watawala wetu wamekuwa wakijisifu ndani na nje ya nchi kwamba hiki ni kisiwa cha amani!

Kisiwa cha amani lakini kina askari wengi kuliko raia; Kisiwa cha amani lakini vigogo wana utajiri wa kukufuru wakati asilimia tisini na tano 95 ya raia ni maskini wa kupindukia?

Kisiwa cha amani lakini magereza yetu yana matabaka, tabaka la 'Five Stars Prison na Negative Stars Prison', watoto wa vigogo wanasoma Ulaya kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu wakati watoto wa wakulima wanasomea chini mbuyu, kisiwa cha amani wakati vigogo wanatibiwa kwenye hospitali za huko Ulaya wao na familia zao, wakati hospitali za hapa hazina dawa na madaktari wanalipwa mishahara midogo sana.

Sawa tumieni ujanja ujanja huo huo mlioweza kuutumia kwa muda wa miaka 52 mkawajengea wananchi wingu la vitisho hadi wakashindwa hata kudai haki zao za kimsingi, kwa kuwaandikia tena katiba nyingine ya upekee wa aina yake, katiba isiyofanana ka katiba nyingine yoyote ile duniani!

Jamii zote duniani zinafanana hasa tukizingatia kwamba binadamu wote ni sawa bila kujali ni mzungu au mwafrika wanafanana kwa mahitaji hivyo tutakuwa wajinga kama tutapuuza wazo la kuchukua katiba mbalimbali za nchi zilizoendelea na kuangalia na kuchukua vipengele muhimu katika katiba zao, vinavyogusa maslahi ya jamii.

Kwa ujumla lazima tufanye hivyo kwa vile kiutaratibu wa mtiririko wa vipengele vya katiba unafanana kote duniani, kama tuliiga kutengeneza katiba toka kwa wakoloni kwa nini leo tunakuwa wagumu wa kuiga kutengeneza katiba nzuri inayokidhi maslahi ya umma?

Wale wale waliojifungia miaka ya sitini wakatuandikia katiba ya Kifalme ndiyo hawa hawa tena wamekuja wanataka wajifungie watuandikie katiba ya upekee zaidi, lakini safari hii wamekuja katika sura mbili tofauti licha ya kwamba ni watu wale wale safari hii wamekuja kama “Tume ya Katiba” na “Jukwaa la Katiba” , hii yote ni kuzuga umma ili hata hapo baadae tukiandikiwa katiba ya upekee serikali ipate sababu za kujitetea kwamba tuliwajumuisha sana raia kwa kila hali.

Je, unaweza kumufahamisha mtu kwa mara ya kwanza kwamba nchi inaongozwa na katiba, na hapo hapo umuulize achangie maoni yake kuhusu katiba mpya, na maoni ya mtu huyo uyatumie kuandika katiba mpya?

Au tulienda vijijini kuhalalisha ufisadi wa kulipana shilingi milioni 300,000,000 kuwa posho za kutafuta katiba mpya!? Huu nauita ni ufisadi miaka 52 ya uhuru kwa vile haiwekani watu 30 waandike katiba ambayo mapungufu yake yanajulikana kwa miaka 52 sasa, na hawaandiki kwa pesa za kawaida hapana, bali kwa kulipana mamilioni ya pesa.

Tungewapa vijana wawili shilingi milioni tatu kila mmoja waliomaliza chuo kikuu wangetuandikia katiba nzuri kwa muda usiozidi miezi mitatu tu! Walioipendelea tume kwa kuipa milioni mia tatu kwa kila mjumbe.

Je, nao wakiiomba tume iwapendelee kwa kulinda baadhi ya vipengele vya katiba visiguswe kwa maslahi yao binafsi, wajumbe watakataa?

Kama mwenzio alikupa kwa kukupendelea na wewe hukusita ukapokea unadhani naye akiomba umpendelee utapata ujasiri wa kukataa? Haya ni maswali ambayo kila Mtanzania anatakiwa ajiulize wakati akisubiri kuandikiwa katiba mpya ya Kipekee.

Katiba ndiyo sheria mama wa kila nchi, sasa kama wanaoandika sheria mama za nchi tayari wameshajihusisha na vitendo vya kifisadi kwa kulipana posho kubwa kuliko hali halisi ya uchumi wa nchi! Je, kwa ustaarabu huu tunaweza kuendelea kusubiri katiba yenye maslahi ya umma!?

Tuendeleeni kusuburi katiba pekee lakini tukae tukijua kwamba wanaotuandikia katiba walishanunuliwa siku nyingi na wale wasiotaka katiba ya umma!

Mwisho kabisa nasema tukijifungia chumbani na kujifanya kuandika katiba pekee tutabakia taifa pekee na kuitwa watu pekee duniani!

Asanteni sana ndugu zangu Watanzania tupende tusipende kuwa huru si rahisi ni ngumu sana hata kama upo chini ya ndugu yako, lakini akishakuwa ameshikilia uhuru wako utapata tabu sana kujinasua.

Dkt. Noordin Jella
Aliwahi kuwa Mhadhiri Chuo Kikuu cha Mzumbe, pia ni mwandishi wa kujitegemea, anapatikana kwa norjella@yahoo.com                                                                                                           Mobile: +255 782 000 131


1 comment:

  1. Safi sana Dkt. Nimependa makala yako. Tatizo kubwa la Watanzania ni uoga kama ulivyosema. Ila naweza kusema haya yote yana mwisho. Shida kubwa ni huo mwisho utakuwaje???? Hawa jamaa wanapata hela nyingi sana na hii inaweza kuwa ni kikwazo cha kuandika katiba mpya. Inashangaza kiongozi kama Malecella anatoa maoni ya katiba ambayo hayafai kutolewa na mtu kama yeye. Tunakumbuka alienda London kutibiwa wakati alipoumwa muda mfupi uliopita. Wazee wa namna hii wanasahau kuwa maskini wa Kitanzania hawezi kwenda hospitali aliyotibiwa yeye. Hii yote ni katiba mbaya ambayo inalinda watu wachache na kuwaacha wengi kwenye linod la umaskini. Licha ya kwamba hatujawahi kuona mchango wa maana wa huyu mzee kwa taifa letu.
    LAKINI MWISHO UPO. Unapokuta nchi ambayo hata viongozi wa majeshi wanatuhumiwa kwa ufisadi basi ujue ndo mwisho huo.

    ReplyDelete