28 January 2013

Kauli ya Mangula iwe kwa vitendo


MAKAMU Mwenyekiti wa CCM,Bw Philip Mangula ameweka msimamo wake dhidi ya wanachama wa chama hicho walioanza kujipitisha kwenye majimbo mbalimbali ya uchaguzi kwa lengo la kujiandaa na uchaguzi ujao.


Wanachama wengi wanaamini kuwa mwisho wa uchaguzi mmoja ndio maandalizi ya uchaguzi mwingine hivyo ni lazima kauli hiyo Bw Mangula iwe kwa vitendo ili wananchi waweze kuamini kwani dhana hiyo imejengeka kwa muda mrefu sasa.

Ndani ya CCM kumekuwa na viongozi wenye nia ya kuwania nafasi za Udiwani,Ubunge na hata Urais lakini kwa kuwa muda wa kufanya hivyo bado basi hatua zichukuliwe kwa wale wanaokwenda kinyume.

Hali hiyo ikiwa itaachwa iendelee itachangia kuwepo mgawanyiko na kuongezeka makundi ndani ya Chama hicho ambayo yamekuwa yakikitafuna kwa muda mrefu sasa.

Tumeshuhudia baadhi ya majimbo ya uchaguzi Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa(NEC) wakijipitisha na kujinadi kuwa wao ndio wabunge huku wakitambua nafasi hizo zinawenyewe hadi mwaka 2015.

Watu wanaonekana kuwa mwiba kwa viongozi walioko madarakani madiwani,wabunge,Rais kwani wamekuwa wakiendesha kampeni za chini kwa chini za kuwahujumu.

Malalamiko dhidi ya wajumbe wa NEC kuwachezea rafu wabunge tayari yamekuwa yakiripotiwa kwenye vyombo vya habari hivyo ni jukumu la uongozi wa juu CCM kuchukua hatua stahiki kwa wanachama hao.

Kampeni hizo zinazoendelea mbaya zaidi zimekuwa pia zikipata baraka za viongozi wa CCM wilaya ambapo baadhi ya maeneo viongozi hao wakuu wa Chama ndio wamekuwa wapiga debe wa wajumbe hao wa NEC kuwahujumu wabunge walioko madarakani.

Ni wazi kuwa wananchi wanaelewa nini walifanya na nani anastahili kuwaongoza kwa wakati huu hivyo si busara kwa viongozi hao wa CCM kutembea na wajumbe wa NEC majimboni na kuanza kuwahuju wabunge na madiwani walioko madarakani sasa.

Badala yake waungane kusimamia kwa vitendo utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ambayo bado kuna udhaifu mkubwa wa usimamizi wa miradi ya maendeleo ambayo mingi imekuwa ikinjengwa chini ya kiwango

Hivyo badala ya kuendesha kampeni za kuhujumiana vema waitumie fursa hiyo kuisimamia Serikali iweze kutimiza wajibu wake kwa wananchi walioiweka madarakani.

Kila kiongozi wa CCM ni vema akatimiza majukumu yake kuliko kutumia vibaya nafasi hizo kuwahujumu viongozi walioko madarakani ambao ndio chaguo la wananchi hadi uchaguzi utakapoitishwa tena mwaka 2015

Kimsingi tunaunga mkono kauli ya Mangula lakini tunahitaji utekelezaji wake kwani ikiwa hautafanikiwa utakisababisha majeraha ndani Chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu.
No comments:

Post a Comment