28 January 2013

TASWA kuwapambanisha Malinzi, Nyamlani


Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimepanga kufanyika mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Februari 15, mwaka huu jijini Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando ilieleza kuwa uamuzi wa kuendesha mdahalo huo, ulifikiwa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika juzi, ambapo pia kilijadili masuala mbalimbali yahusiyo chama hicho.

Alisema tayari kikao kimeiagiza Sekreterieti ya TASWA, ifanye maandalizi ya mdahalo huo kwa kuzungumza na vituo vya televisheni, ili uweze kuoneshwa moja kwa moja ili wananchi waweze kuwasikia wagombea hao.

Pia alisema mazungumzo ya awali na wadhamini mbalimbali yameanza kuweza kufanikisha tukio hilo la kuendesha mdahalo wa 'live' kwenye televisheni. Nafasi ambazo wahusika watafanyiwa mdahalo ni Rais na Makamu wa Rais.

Mhando alisema TASWA, imekuwa ikifanya mdahalo kwa wagombea wa nafasi za juu kwenye uchaguzi wa TFF, ilifanya hivyo mwaka 2001 na mwaka 2004 ingawa haukuwa wa live, ikafanya wa live mwaka 2008, hivyo TASWA itafanya mawasiliano na TFF ili iweze kupata msaada wa karibu kufanikisha jambo hilo.

"Tunaamini ushirikiano uliopo kati ya TFF na TASWA utasaidia kwa namna fulani kufanikisha jambo hilo, ambapo mdahalo utahusisha waandishi wa habari waandamizi wa michezo, wahariri wa baadhi ya michezo na wadau wachache wa soka," alisema.

Katibu huyo alisema Kamati ya Utendaji, imesisitiza katika kikao chake kwamba uchaguzi wa TFF haimuungi mkono mgombea yeyote na haina mpango wa kumuunga mkono mgombea yeyote, hivyo TASWA inaonya kama kuna baadhi ya wagombea wenye ndoto za kutaka kutumia mgongo wa TASWA, kwamba chama kinawaunga mkono ili wapate mteremko kufikia malengo yao hazitatimia.

"Kama kuna kiongozi au mwanachama wa TASWA ambaye anamuunga mkono mgombea yeyote wa TFF, huo utakuwa msimamo wake binafsi si wa chama na kama atahusisha chama kwa namna yoyote, atakuwa anakosea na hatutasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa katiba ya chama," alisema.

No comments:

Post a Comment