28 January 2013

Tanzania kunufaika na miradi mitatu mikubwa kutoka China


Na Anneth Kagenda

TANZANIA inatarajia kuneemeka na miradi mikubwa mitatu kutoka nchini China ambayo itagharimu zaidi ya sh. bilioni 28.2 za kitanzania ukiwamo mradi wa chakula ambapo chakula hicho kitasambazwa katika maeneo yote nchini hasa yale ya vijijini ili kupunguza tatizo kubwa lililopo.


Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Waziri wa Fedha, William Mgimwa wakati wa kutiliana saini  fedha za miradi hiyo na Ubalozi wa Japan nchini Tanzania kuhusu.

Alisema mradi huo wa chakula ambao utatumia sh. bilioni 6.92 utaweza kutatua tatizo kubwa lililopo hasa maeneo ya vijijini na kwamba watu sasa wataweza kuendelea kuzalisha na kupata chakula kingi mara tu utakapoanza kuingia nchini.

"Kutokana na kwamba leo tunasaini hatukuweza kuchanganua ni maeneo yapi tutapeleka, lakini ninachojua ni kwamba maeneo yote ndani ya nchi yasiyokuwa na chakula yatafikiwa mara tu mradi utakapokuwa umefika na sasa kinachofuata ni utekelezaji," alisema Waziri Mgimwa.

Aidha aliutaja mradi wa pili kuwa ni ule wa upanuzi barabara ya Gerezani na Bandari kati ya Kamata na barabara ya Kilwa ambao utatumia sh. bilioni 20 na lengo la upanuzi likiwa ni kutokana na kwamba kwa kipindi kilefu kumekuwa na tatizo la kimawasiliano kutokuwa mazuri hasa kwa watu wanaoishi maeneo ya Mbagala wanapotaka kuingia mjini mtu anaweza kukaa barabarani zaidi ya masaa mawili.

Lakini kwa upande wa mradi wa tatu ambao utatumia sh.bilioni 1.20 ni ujenzi wa daraja eneo la Tazara, ambapo zitajengwa barabara za juu na kusema kuwa eneo hilo pia lina tatizo kubwa la foleni, hivyo baada ya ujenzi huo watu wataweza kufanya shughuli zao haraka na badaye kuweza kukuza uchumi zaidi kuliko hali ilivyo sasa.

"Niweke sawa kwamba miradi na misaada hii ambayo imekuwa ikitolewa na Japani ni kutokana na historia tuliyonayo ya mahusiano mazuri toka miaka ya 1960 hasa katika mambo ya kiuchumi," alisema Mgimwa.

Naye Balozi wa Japani nchini Masaki Okada alisema kuwa miradi hiyo inayotarajiwa kutekelezwa nchini hapa italeta tija kutokana na kwamba imelenga zaidi katika kusaidia kukuza uchumi.

Alitolea mfano kuwa kwa wale waliokuwa wanatumia masaa mawili wakiwa barabarani hasa ile ya Kilwa baada ya mradi kukamilika wataweza kutumia dakika 30, kwamba hiyo inaonesha ni kwa jinsi gani miradi hiyo itasaidia.

"Lakini ninaweza kusema kuwa Japan imeendelea kutoa misaada na itaendelea kufanya hivyo, kwani ushirikiano wetu ni mkubwa sana, lakini ikumbukwe kwamba project hizi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi husika hivyo tutatumia nguvu zote ili kuhakikisha inakamilika na kwa wakati," alisema.

No comments:

Post a Comment