28 January 2013

Rais Kikwete kutetea ripoti utawala bora leo


Na Hassan Abbas, Addis Abbas

Rais Jakaya Kikwete leo Jumamosi anatarajiwa kuiwasilisha na kuitetea
Ripori ya hali ya Utawala Bora mbele ya viongozi wenzake wa nchi za Afrika
zinazoshiriki  katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).


Wakati Rais Kikwete akitarajiwa kuitetea Ripoti hiyo leo, jana, Ijumaa,
Waziri Bernard Membe ambaye Wizara yake ndiyo inayoratibu shughuli za APRM
nchini Tanzania alitarajiwa kuanza utetezi huo mbele ya Mawaziri na maofisa
wengine waandamizi zaidi ya 100 kutoka nchi mbalimbali za Afrika katika
mkutano wa utangulizi siku ya Ijumaa.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib, Mkutano wa
Ijumaa ulikuwa ni wa maandalizi kabla ya kikao cha Marais cha leo.

Kupitiwa kwa ripoti ya Tanzania kumekuja wakati muhimu katika historia ya
Afrika, APRM na Tanzania yenyewe: Mkutano wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi hizo
unaoanza Jumapili utabeba kauli mbiu ya “Umajimuni wa Kiafrika na Uhuisho
wa Afrika; APRM inatimiza miaka 10, Tanzania inaingia katika mkutano huo
ikiwa imeanza safari nyingine ya miaka 50 ya kujenga nchi.

Kabla ya Rais Kikwete kuwasilisha ripoti hiyo ambapo pia Rais Michael Sata
wa Zambia naye atawasilisha na kuitetea ripoti ya nchi yake, katika
kuadhimisha miaka 10 ya APRM kuwatumikia watu wa Afrika, kutakuwa na
mdahalo maalum utakaojadili changamoto za APRM na jinsi Afrika inavyoweza
kukabiliana na changamoto za migogoro mbalimbali.

Viongozi wa Afrika waliothibitisha kushiriki katika mdahalo huo ni
Hailemariam Desalegn, (Waziri Mkuu wa Ethiopia); Abdelaziz Bouteflika
(Algeria), Dkt. Boni Yayi, (Benin), Armando Emilio Guebuza (Msumbiji), Dkt.
Goodluck E. Jonathan (Nigeria), Paul Kagame (Rwanda), Jacob Zuma (Afrika
Kusini) and Yoweri Kaguta Museveni (Uganda).

Katika mkutano huo pia Marais wan chi nne za Cape Verde, Chad, Equatorial
Guinea na Tunisia wanatarajiwa kusaini mkataba wa kujiunga na APRM hivyo
kufanya nchi ambazo zitakuwa ni wanachama wa Mpango huo kufikia 35 kati ya
nchi 54 za AU.

Tayari ujumbe wa APRM Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa
la Usimamizi, Prof. Hasa Mlawa, mjumbe wa Baraza hilo anayewakilisha Bunge
la Jamhuri ya Muungano, John Magalle Shibuda na maofisa wengine waandamizi
wa APRM wamekwishawasili jiji hapa kwa maandalizi ya mkutano wa leo.

Mpango wa APRM uliasisiwa miaka 10 iliyopita na Wakuu wa Nchi za Afrika kwa
lengo la kuanzisha taasisi itakayokuwa na majukumu ya kufanya tathmini za
mara kwa mara za hali ya utawala bora miongoni mwa nchi wanachama ili
kuwashirikisha wananchi wao katika kujikosoa na kujisahihisha.

No comments:

Post a Comment