03 January 2013

TAKUKURU isisubiri kukumbushwa wajibu



MAKAMU Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Said Arfi, ameitaka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Katavi kuchunguza tuhuma zilizotolewa dhidi yake kuhusiana na kupokea rushwa kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.


Arfi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, alitoa kauli hiyo wiki hii wakati wa mkutano wake wa hadhara.

Kauli hiyo ya Arfi ni ya kwanza kuitoa tangu alipotuhumiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), Laurent Mangweshi, katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya chama hicho kilichofanyika Desemba 16, mwaka huu.

Inadaiwa katika kikao hicho Mangweshi anadaiwa kusema kuwa Arfi alipokea rushwa kutoka kwa Waziri Mkuu. "Mimi ni mwadilifu na sipendi kuchafuliwa na ndiyo maana baada ya tuhuma hizo siku iliyofuata nilikwenda TAKUKURU kueleza shutuma hizo dhidi yangu ili waweze kuzichunguza."

Kauli hiyo iliyotolewa na Arfi kwetu sisi tunaiona kama changamoto kwa TAKUKURU na si kwa maofisa wa mkoa wa Katavi peke yake, bali kwa chombo hicho nchi nzima.

Tunasema hivyo kwa kutambua kuwa katika maeneo mengine taasisi hiyo imekuwa ikichelewa kufanyia kazi tuhuma za rushwa zinazowakabili watu mbalimbali licha ya kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

Kwa msingi huo tunaiomba taasisi hiyo isisubiri watu waende kulalamika kwake kama alivyofanya Arfi, badala yake kila inapoonekana dalili ya vitendo vya rushwa au watu kutuhumiwa basi hatua zichukuliwe mara moja.

Tunatambua kuwa taasisi hiyo inafanyakazi kubwa na nzuri licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za uhaba wa rasilimali watu, lakini changamoto hizo ziwe chachu ya kuongeza ari ya utendaji kazi wake.

Kwa kufanya hivyo watu wengi watazidi kuwa na imani na chombo hicho ndani ya jamii. Kinyume na hivyo taasisi hiyo haitaaminika hasa pale mtu anaposimama na kutoa tuhuma nzito zinazogusa kiongozi wa juu serikali na chombo hicho kikabaki kimya bila kuchukua hatua, hapo lazima kila mwananchi ajiulize maswali mengi yaliyojaa mashaka.

Lakini maswali hayo hayatakuwepo iwapo tuhuma zinazotolewa au malalamiko yatafanyiwa kazi mara moja. Kwetu sisi tunaamini kuwa hicho ndicho kitakuwa kipimo cha kwanza cha kupima uwajibika wa taasisi hiyo.

Maofisa wa taasisi hiyo wawe ni watu wa kunusa kila penye viashiria vya rushwa ndani ya taifa letu ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi malalamiko yakiwemo yale yanayotolewa na viongozi wa ngazi mbalimbali hasa yaliyojaa mashaka kwenye mikataba ya uwekezaji.

Kwa kufanya hivyo wananchi watanufaika na kuwepo kwa taasisi hiyo na kwa kujiona inagusa maisha yao.

No comments:

Post a Comment