03 January 2013

Uchimbaji gesi waibua mapya *Wananchi Mtwara waapa kuharibu miundombinu *Wizara ya Nishati yagoma kuzungumza chochote


Na Waandishi Wetu

SIKU moja baada ya wananchi mkoani Mtwara kufanya maandamano makubwa ya kupinga kusafirishwa gesi asilia
kwa njia ya bomba kutoka mkoani humo hadi Dar es Salaam,
sakata hilo limeanza kuchukua sura mpya.


Hali hiyo inatokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kumtaka Rais Jakaya Kikwete, azungumzie hali halisi juu ya mikataba ya gesi na matumizi yake kama alivyofanya wakati akizindua ujenzi wa miundombinu yake hivi karibuni
jijini Dar es Salaaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mbunge wa Ubungo ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madinia, Bw. John Mnyika, alisema matokeo ya maandamano hayo ni baada ya yeye kutaka ufafanuzi wa fedha za mkopo zaidi ya sh. trilioni moja zilizotolewa na Serikali ya China.

Alisema fedha hizo zilikopwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia lakini Serikali imeshindwa kutoa majibu licha ya msingi wa hoja yake kuridhiwa na Bunge.

Bw. Mnyika ambaye pia ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, alisema ni muhimu Rais Kikwete akaingilia kati tatizo lililopo na kuwaeleza wananchi hasa wakazi wa Mtwara juu ya faida ambayo wataipata kutokana na uzalishaji gesi hiyo mkoani humo.

“Rais Kikwete anapaswa kulisemea hili katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa wananchi kama ilivyo kawaida yake, Julai 27 mwaka huu. nilihoji bungeni kuhusu mikataba ya gesi.

“Tanzania imeanza kuchimba gesi mwaka 2004 lakini kulikuwa na ufisadi wa hali ya juu na Bunge liliridhia hilo lakini hadi leo hakuna majibu rasmi kutoka serikalini,” alisema Bw. Mnyika.

Aliongeza kuwa, hadi sasa hakuna chombo kinachoisimamia Serikali katika nishati hiyo hivyo ni vyema Spika wa Bunge
Bi. Anne Makinda, akaunda kamati ya kufuatilia suala hilo.

Alisema msimamo wa CHADEMA ni kuitaka Serikali itoe majibu juu ya maandamano hayo na madai ya wananchi kuhusu gesi asilia kwani wao walishasema bungeni lakini hakuna majibu hadi sasa.

“Wananchi wa Mtwara wanapaswa kuambiwa ukweli kuhusu gesi yao lakini kwa sababu Serikali ipo kimya ndio maana wameamua kuandamana na kudai haki yao.

“Serikali iweke hadharani mikataba ya utafutaji gesi, uchimbaji, usafirishaji na kufafanua itawanufaisha vipi wananchi, hata gesi
ya Songosongo ambayo tayari imeanza kusafirishwa nayo pia itolewe ifafanuzi wa faida ambayo wananchi wataipata,” alisema.

Alisema mapato ya ukusanyaji kodi inayotokana na uchimbaji wa gesi bado kitendawili kwani Tanzania imepunjwa dola bilioni moja tangu ilipoanza kuchimba gesi na jambo hilo lipo wazi.

Wananchi Mtwara wacharuka

Katika hali isiyo ya kawaida, wananchi mkoani Mtwara wameamua kuunda kamati maalumu ambayo itakutana na Rais Kikwete kupata muafaka wa madai yao na kama muafaka huo utashindikana, wapo tayari kuhakikisha mradi huo haufanikiwi.

Taarifa zilizotufikia kutoka mkoani humo, zinadai baada ya wananchi kukosa majibu ya Serikali ya Mkoa juu ya madai yao, wanakusudia kuunda kamati ambayo itafikisha kilio chao jinsi
watakavyonufaika na gesi hiyo.

“Jana (juzi), tumefanya maandamano lakini cha kusikitisha, Mkuu wa Mkoa amekataa kuyapokea na kusema chochote kuhusu madai ya wananchi na kamati tutakayounda isipopewa majibu ya kuridhisha, tutaharibu miundombinu ya mradi huu,” walisema.

Wananchi hao walidai kuwa, kati ya mambo wanayolalamikia ni gharama kubwa za kuunganishiwa umeme na kuwa mzigo kwao pamoja na upatikanaji wa fomu kuwa na urasimu mkubwa.

Waliongeza kuwa, watu wanaonufaika na gesi hiyo ni wale waliojenga pembezoni mwa barabara kuu ndani ya mita 30 na
kudai kuwa, Serikali haikuweka mazingira mazuri kwa wananchi ambao wanaishi mbali na barabara hiyo.

“Uwamuzi wa kupeleka gesi Dar es salaam unapingana na tamko
la Rais kikwete alilolitoa kwenye ziara yake mkoani hapa mwaka 2009 na kudai Mkoa ujiandae kuwa ukanda wa viwanda.


“Tunataka vinu vya gesi vijengwe hapa Mtwara ambako kuna maeneo ya kutosha tofauti na Dar es salaam, viwanda vikubwa vijengwe hapa ili kutoa ajira kwa wananchi,” walisema.

Walidai kuchoshwa na mikoa ya Kusini kuwa nyuma kimaendeleo ambapo umoja wao unalenga kuhakikisha rasilimali ya gesi haitoki kwenda kokote kabla haijanufaisha wazawa.

Inadaiwa kuwa, wananchi hao tayari wameunda kamati ya watu wanne ikiongozwa na Makamu mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Siasa mkoani humo, Bw. Hassan Msata na Msemaji Mkuu wa msafala huo atakuwa  Bw. Hamza Licheta.

Jitihada za kuupata uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini ili kuzungumzia madai ya wananchi, hazikufanikiwa baada ya watendaji wa Wizara hiyo kugoma kuzungumza chochote.

Habari hii imeandikwa na David John, Cornel Antony na Goodluck Hongo.

No comments:

Post a Comment