31 January 2013

Stars yazitosa Rwanda, Congo *Sasa kucheza na CameroonNa Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema lilipata maombi ya kucheza na nchi nne tofauti katika 'FIFA date', lakini imeamua kuachana nazo kutokana na kushindwa kufikia muafaka na kuamua kuikubalia Cameroon.


Nchi hizo ni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Rwanda, Swaziland, Rwanda na Equatorial Guinea ambazo zote zilitaka mechi zichezewe katika ardhi za nyumbani kwao.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema kabla ya kufikia muafaka na Cameroon, kulikuwa na nchi zingine nne ambazo ziliwaomba kucheza nazo lakini, kadri siku zilivyokuwa zinasonga hazikuonesha dalili nzuri ya muafaka.

"Awali kocha Kim (Poulsen), alipendekeza tucheze mechi za ugenini kwa ajili ya wachezaji kupata uzoefu, lakini tulifanya mawasiliano na timu hizo mpaka dakika za mwisho, hata hivyo hazikuonesha dalili nzuri kwani kuna vitu tulihitaji wathibitishe zikawa zinasuasua," alisema Osiah na kuongeza;

"Kutokana na hilo tukaamua ni bora tucheze na Cameroon, ambao walionesha nia ya dhati ya kutaka kucheza na sisi, lakini hapa nyumbani na wanazidi kusisitiza kwamba lazima waje Tanzania."

Alisema timu hiyo inatarajiwa kutua nchini Februari 3, mwaka huu ikiwa na msafara wa watu 36, 12 kati yao ni viongozi na waliobaki ni wachezaji na benchi la ufundi.

Katibu huyo alisema mechi hiyo kwa kuwa itachezwa Februari 6 mwaka huu ambayo itakuwa siku ya kazi, itachezwa kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na tayari wameshawasiliana na serikali kuhusu ulinzi na mambo mengine, kwa sasa kinachosubiriwa ni vikao kuanza.

Alisema kocha Kim, atatangaza kikosi chake leo kitakachocheza na Cameroon na kambini kitaingia Jumamosi na wengine Jumapili, ambapo Jumatatu wataanza mazoezi rasmi.

Alisisitiza kwamba katika mkataba waliongia na Cameroon kwa mujibu wa kanuni za FIFA (Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu), katika siku za FIFA ni lazima timu zichezeshe vikosi vyao vya kwanza na si vinginevyo.

Alisema timu hiyo itatua nchini kwa mafungu, ambapo kutakuwa na kundi litakalotokea Afrika Kusini likiwa na kocha na viongozi wengine, kuna wachezaji wanaocheza Ulaya ambao watakutana Amstadam, Uholanzi na wengine wataondokea jijini Younde.

Katika hatua nyingine, Osiah alisema tayari wameshaiandikia barua TP Mazembe ya DRC, kuhusu kuwahitaji wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu na ana imani kwamba wataruhusiwa mapema.

No comments:

Post a Comment