14 January 2013

Serikali yatoa chakula cha msaada Igunga



Na Abdallah Amiri, Igunga

SERIKALI imetoa chakula cha msaada tani 1,790 za mahindi katika Wilaya ya Igunda, mkoani Tabora na fedha sh. milioni 89,700 ili kiweze kusambazwa kwa wananchi wilayani humo.

Msaada huo umetokana na ombi la wananchi Kijiji cha Makomero, Kata ya Igunga, mkoani humo kumweleza Rais Jakaya Kikwete tatizo la njaa walilonalo wakati akiwa katika ziara ya kikazi.

Rais Kikwete lipokea ombi la wananchi hao na kusisitiza kuwa, hakuna mwananchi ambaye atakufa na njaa kwa sababu Srikali
ina chakula cha kutosha kwa ajili ya kuwapa wananchi wake.

Akizungumza na wandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Mkuu
wa Wilaya hiyo, Bw. Elibariki Kingu, amesema chakula hicho kimepelekwa katika muda muafaka ambapo wananchi wa Igunga wamefurahishwa kitendo cha Serikali kukubali ombi lao pamoja
na Rais Kikwete kutekeleza ahadi yake katika kipindi kifupi.

“Nawaomba wananchi wakitumie chakula hiki vizuri ili kiweze kuwasaidia kwani wengi wao hawakuwa na chakula hivyo walikuwa wakiacha shughuli za kilimo na kwenda kutafuta chakula,” alisema.

Kwa upande wao, wananchi hao walimuomba Bw. Kingu kusimamia vizuri mchakato wa ugawaji chakula hicho.

Mkazi wa kata hiyo, Bw. Moka Changarawe, alisema baadhi ya viongozi si waadilifu pindi Serikali inapotoa misaada kama hiyo akitolea mfano wa chakula kilichotolewa mwaka 2011, ambapo
baadhi ya viongozi walijinufaisha wenyewe badala ya walengwa.

Kutokana na ombi hilo, Bw. Kingu aliwaonya watendaji wa serikali wilayani humo na kusema kuwa, hayupo tayari kuona Mtendaji yoyote akifanya hujuma katika chakula hicho cha msaada.

“Mtendaji ambaye atabainika kufanya hivyo, atakuwa amejifuta kazi na atafikishwa mahakamani nawaomba viongozi wote wa vyama vya siasa kutumia muda mwingi kuhamasisha suala la kilimo badala ya kupoteza muda mwingi kuzungumzia siasa,” alisema.

No comments:

Post a Comment