21 January 2013
Serikali kuendelea kushirikiana na Misri kuboresha huduma ya maji
Na Jovin Mihambi, Maswa
WAZIRI wa Maji Profesa Jumanne Maghembe amesema,
serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Watu wa Misri katika kuboresha huduma ya maji hususani kwa wananchi waishio kwenye vijiji ambavyo vimekuwa vikikumbwa na janga la ukame ili waweze kupata maji
salama.
Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa sherehe ya kukabidhi
visima 30 vya maji salama ambavyo vilichimbwa katika wilaya sita ambazo
zimekuwa na uhaba wa maji unaosababishwa na ukame. Sherehe hiyo ilifanyika
katika kijiji cha Mandang’ombe, kata ya Lalago, wilayani Maswa hapo Januari, 17
mwaka huu na wilaya ya Maswa kuwakilisha wilaya zingine ambazo zimepata msaada
huo.
Alisema kuwa serikali Jamhuri ya Watu wa Misri kwa kutambua
umuhimu wa Watanzania hususani waishio kwenye vijiji ambavyo vimekuwa vikikubwa
na ukame, ilitoa fedha zinazofikia sh.billioni 2.4 kwa ajili ya kuchimba visima
thelathini katika wilaya za Same, Kiteto, Maswa, Magu, Bunda na Tarime na
katika upande wa vijiji vya Maswa vilichimbwa visima sita.
Profesa Maghembe alisema kuwa wanavijiji ambao wamechimbiwa
visima hivyo, wataweza kuondokana na shida ya maji huku akiwalenga wanawake
ambao mda mwingi wamekuwa wakiutumia kwa kusafiri mwendo mrefu kwa ajili ya
kutafuta maji na kuasha kufanya shughuli zingine za maendeleo katika jamii na
kuwataka kutunza visima hivyo ili huduma yake iwe endelevu ili kushawishi wafadhili
kuendelea kutoa
msaada huo katika sehemu nyingine yenye matatizo kama hayo.
Naye Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa serikali ya Misri Profesa
Dk. Mohamed Bahaa El-Din Ahmed katika hotuba yake, alisema kuwa serikali ya
Watu wa Misri licha ya kutoa ufadhili wa kuchimba visima, nchi hiyo itaendelea
kushirikiana na serikali ya Tanzania katika Nyanja zingine na kutoa ufadhili wa
kufundisha wataalamu wa kilimo cha umwagiliaji, elimu, afya na fani zingine
kulingana na mahitaji ya Tanzania.
“Tanzania na Misri zimekuwa zikishirikiana katika Nyanja za
siasa, maji, kilimo cha umwagiliaji na afya tangu enzi za marehemu Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na marehemu Gamal Abdel Nasser ambaye
alikuwa Rais wa Misri. Na katika miaka ya sitini na sabini, Tanzania ilikuwa
moja ya nchi za Bonde la Mto Nile zilishoshiriki kwenye mradi wa ukusanyaji wa
takwimu za maji ambao ulijulikana “Lake Victoria Hydrometric Project ambao
ulifadhiriwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa hivyo ushirikiano huo
ni mwendelezo wa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Misri”, alisema Prof.Dk
Mohamed Bahaa El-Din Ahmed.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw Pascal Mabiti, alisema kuwa
mkoa wa Simiyu ni mojawapo ya mikoa ya Tanzania ambao unazalisha pamba kwa
wingi hivyo kuiomba serikali ya Tanzania kushirikiana na serikali ya Misri ili
kuleta wawekezaji katika kilimo cha pamba na kujenga viwanda vya kusokota nyuzi za
pamba pamoja na kuwekeza katika viwanda vya
nyama kutokana na mkoa huo kuwa na mifugo mingi na wafugaji wakibakia maskini
kutokana na mifugo yao kulanguliwa na wafanyabiashara kwa bei ndogo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment