18 January 2013

Polisi Kishapu watupiwa tuhuma nzito


Na Suleiman Abeid, Shinyanga

BAADHI ya viongozi katika Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, wamelitupia lawama Jeshi la Polisi, wilayani humo kutokana na baadhi ya askari wake, kudaiwa kushirikiana na wahalifu pamoja
na kupokea rushwa.

Tuhuma hizo nzito zilitolewa juzi katika kikao maalumu kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Wilson Nkhambaku ambacho kilishirikisha madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Williamson Diamonds Ltd wa Mwadui na Wenyeviti wa Vitongoji kutoka katika kata hizo.

Kikao hicho kiliitishwa kwa ajili ya kujadili tukio la hivi karibuni
la kundi la watu wapatao 200 maarufu kwa jina la 'Wabeshi', ambalo lilivamia eneo la mgodi huo na kuiba mchanga unaohisiwa kuwa na madini ya almasi.

Akizungumzia tatizo hilo, Diwani wa Kata ya Songwa, Bw. Mohamed Shaban, alisema baadhi ya polisi wamekuwa chanzo kikubwa cha uhalifu unaoendelea kufanyika katika eneo hilo.

Alisema yeye binafsi hawezi kulipa asilimia 100 jeshi hilo katika utendaji kazi wake kwani mara nyingi polisi wanapokamata wahalifu katika eneo la mgodi huo, huwaachia baada ya
kupewa kitu kidogo 'rushwa'.

Alisema hali ya ulinzi katika eneo la mgodi kwa sasa si nzuri baada ya kundi hilo kuanza kujihami kwa kutumia mawe ili kujikinga na risasi za walinzi wa eneo hilo.

“Tabia ya baadhi ya walinzi wa mgodi huu kutumia silaha za moto kwa watu wanaowatuhumu badala ya kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria si cha kiungwana kabisa,” alisema.

Akijibu tuhuma hizo, Mkuu wa Polisi wilayani humo, (OCD) Richard Abwao, alisema hawezi kukanusha au kukiri juu ya tuhuma zilizotolewa kwa askari wake bila ya kufanya uchunguzi wa kina.

Alionesha kushangazwa na kauli zinazodai kuna polisi wanaopewa fedha ili kuwaachia watuhumiwa wanaokamata wakati viongozi hao wakidai wabeshi hivi sasa wanatumia mawe kuwapiga polisi ili wasiweze kukamatwa.

“Siamini kama kweli kuna polisi wanaopewa fedha, kama madai yenu yana ukweli kwa nini wapigwe na hawa wabeshi...polisi si wachafu kiasi hicho kwani Serikali inatumia fedha nyingi katika suala zima la ulinzi,” alisema Kamanda Abwao.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Nkhambaku aliwaomba viongozi hao kuhakikisha wanasimamia suala zima la sheria katika maeneo yao.

No comments:

Post a Comment