18 January 2013

Katibu CCM achunguzwa na TAKUKURU


Na Patrick Mabula, Kahama

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, inamchunguza Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), wilayani humo, Bw. Masoud Melimeli.


Bw. Melimeli anatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kuomba
na kupokea rushwa kwa wapangaji waliopanga kwenye vibanda
vya biashara wilayani humo vinavyomilikiwa na CCM ambavyo vimejengwa katika Ofisi Kuu ya chama wilayani humo.

Tuhuma hiyo zimetokana na tukio la hivi karibuni ambalo chama hicho wilayani humo, kiliwaondoa baadhi ya wapangaji wake ambao walidaiwa kukosa sifa za upangaji na wengine kukiuka mikataba hivyo Bw. Melimeli anadaiwa kukusanya pesa ili baadhi ya
wafanyabiashara waweze kupewa upendeleo.

Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Bw. Mabala Mlolwa, alikiri taasisi hiyo kumchunguza Bw. Melimeli kutokana na malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya watu waliodai kumpa pesa ili awape sehemu ya kufanyia biashara wakati chama hicho kikitekeleza mkakati wa kuwaondoa wafanyabiashara waliokiuka mikataba.

“Mimi kama kiongozi wa chama ngazi  ya Wilaya, tuliamua tuhuma hizi zifanyiwe uchunguzi na TAKUKURU pamoja na kulitolea maaamuzi kwa sababu mtuhumiwa ni kiongozi wa ngazi yangu kwenye chama,” alisema Bw. Mlolwa.


Kwa upande wake, Bw. Melimeli alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema, tuhuma dhidi yake zimekuwa zikipikwa na baadhi ya viongozi wenzake ndani ya chama hicho kutokana na makundi
yaliyopo wilayani humo.

“Madi yote yanayotolewa dhidi yangu ya uongo na uzushi ambao haufai, wananichafulia jina langu kutokaana na baadhi ya viongozi kuwa na hasira za wagombea wao kushindwa katika uchaguzi uliopita mwaka 2012,” alisema Bw. Melimeli.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM wilayani humo, Bw. Michael Bundalla, alikiri Bw. Melimeli kuchunguzwa na TAKUKURU.

No comments:

Post a Comment