14 January 2013

Ongezeko la majengo si maendeleo ambayo tunayahitaji


WATAWALA na baadhi ya wananchi, wanatumia nguvu kubwa kufafanua maendeleo kwa kuyahusisha na ongezeko majengo ya kifahari na magari barabarani.

Miaka ya 1980, mashirika ya misaada yalifanya jitihada kubwa za kuhamasisha maendeleo na kuongeza misaada kwa nchi maskini.


Kimsingi juhudi za mashirika hayo hazikuzaa matunda bali ni njia za kufanikisha matamanio na mahitaji ya binadamu katika nyanja za weledi, hisia, imani, mitazamo, mapato na mahusiano.

Baada ya mashirika hayo kulitambua hilo, miaka ya 1990, harakati na mitazamo ya kusaidia maendeleo ikaanza kuzingatia vigezo vya kijamii na utamaduni.

Sisi tunasema kuwa, takwimu za ukuaji uchumi wetu si majengo ya kifahari na magari mengi barabarani bali hivyo ni viashiria tu vya maendeleo lakini siyo tafsiri sahihi wala vigezo sahihi.

Taifa linaweza kuwa na pato kubwa la ndani lakini wananchi wake wanasumbuliwa na maradhi, njaa na migogoro isiyoisha.

Unaweza kukuta mtu anaishi katika nyumba ya kifahari na kutembelea gari lakini hana maarifa kichwani. Nchi nyingine zinaweza kuwa na takwimu nzuri za kukua kwa uchumi lakini wananchi wake wanakufa kutokana na kusumbuliwa na maradhi.

Ukweli ni kwamba, hakuna binadamu mwenye njaa anayeweza kushiba takwimu za kukua kwa uchumi. Kimsingi maendeleo hayaangaliwi kwa kigezo kimoja au viwili.

Jamii inapaswa kutambua kuwa, suala la maendeleo linapaswa kuangaliwa kwa ujumla wake likihusisha takwimu za viwango vya maisha ya watu, mtaji jamii, amani, utulivu, upatikanaji wa huduma bora za jamii, ushirikiano na maelewano.

Imani yetu ni kwamba, maendeleo ni ustawi wa maisha ya watu. Jamii inapaswa kupata mahitaji muhimu ya kuishi kama chakula bora, maji, huduma za afya, malazi na elimu.

Hakuna sababu ya wanasiasa kupiga debe na kujigamba kuwa hivi sasa tumepiga hatua kubwa ya maendeleo wakati familia nyingi hazipati huduma muhimu.

Wapenda maendeleo, wanapaswa kubadilishana taarifa na kuhimizana ndani ya jamii ili kila mmoja kwa nafasi yake, atoe mchango wake kwa maendeleo yake, familia na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment