14 January 2013

Lugha kali za wauguzi kwa wagonjwa zikomeshwe


Na Esther Macha

KAMA nguzo ya familia, mwanamke anatakiwa kuheshimiwa na kuthaminiwa kutokana na majukumu yake ili kufanya vizuri zaidi.

Wanatakiwa kupewa nafasi ya pekee ili kuwapa nguvu zaidi ya kusimamia waliyoanzisha kwa manufaa ya jamii.


Kutokana na heshima yao na majukumu waliyonayo katika Taifa, walitakiwa kulindwa lakini hali hiyo imekuwa tofauti na wanawake kuonekana ni watu wa chini daima na wanaodharauliwa.

Laiti kama wengi wangejua maana ya mwanamke sidhani
kama kungekuwepo na dharau kwao, kwani bila wao tusingekuwepo hapa.

Binafsi nimeumia kwa kitendo cha mwanamke mwenzetu
kudhalilishwa kwa kujifungulia kwenye korido  ambalo linapita watu wengi mpaka watoto wadogo wote wakiwa wanashuhudia tukio hilo.

Sijajua kwanini ilifikia hatua hiyo koridoni wakati manesi wa wodi wa wazazi walikuwepo hakika sijapenda kitendo
hiki kwani ni cha udhalilishaji. Hali kama hii inatakiwa ikomeshwe.

Kutokana na kitendo hiki kuna kila sababu wahusika wakuu katika hospitali ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro wachukuliwe hatua za kisheria, sioni sababu ya wao kukaa kupiga soga wakati wapo kazini kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa.

Kulikuwa na sababu gani za wao kukaa ndani  na kuchelewa kumpokea mgonjwa na kumpa huduma zinazostahili hadi afikie hatua ya kujifungulia nje ya wodi?

Tatizo lilopo ni kwamba baadhi ya wauguzi wamesomea kazi hizo lakini hawana wito na kazi hiyo na hivyo kubaki  wakifanya kazi hiyo ili mradi waweze kuendesha maisha, ndio maana wanakuwa na roho ya ukatili kiasi hicho kwa wanawake wenzao.

Kumekuwepo na matukio mengi ya kutoa lugha chafu kwa wagonjwa na huduma mbovu sehemu mbalimbali lakini wahusika hawachukuliwi hatua stahiki licha ya kufanya
makosa hayo.

Nadhani kinachofanyika hapa ni ile tabia ya kulindana
kazini wakati wananchi wanazidi kufa kwa sababu ya watu wachache wasiofuata maadili ya kazi yao kuwa wanatakiwa wafanye nini.

Nionavyo kuhusu udhalilishaji huu wahusika wachukuliwe hatua, isiwe kimya kama ilivyozoeleka siku zote kwani hali hii ikiendelea wanawake wengi watapoteza maisha kwa uzembe wa watu wachache ambao wapo kimaslahi zaidi kuliko utu wa binadamu.

Miaka ya nyuma kazi ya uguuzi ilikuwa na maadili sana lakini
sasa kazi hii imekuwa haina maadili hata kidogo kwani hata ukienda hospitali unatakiwa kutoa rushwa ili upate huduma mapema.

Hali hii ipo hata kwa madakatari kwani hawana tofauti na
manesi katika baadhi ya hospitali za rufaa zimegeuzwa kama taasisi kuchumia fedha za walalahoi, sasa kuna sababu gani ya hospitali hizo kuwepo wakati huduma hakuna? na
ikiwepo lazima ulipie hata kama ni bure.

Ifike wakati wauguzi katika wodi za wazazi wawe na ubinadamu kwa wanawake wenzao wasiangalie hali ya mtu ndipo watoe huduma kwa mjamzito kwani si wote ambao wana uwezo wa kuwapatia fedha.

Kitendo cha kumdhalilisha mjamzito huyo mmejisikiaje? Ungefanyiwa wewe? Tuwe na ubinadamu kwa kupendana na kusaidiana.

Lakini pia kutokana na maumivu makali aliyopata kwa muda mrefu mwanamke huyo alipoteza mtoto wake huu ni unyama.

Hivi karibuni  Mkazi wa Morogoro aliyefahamika kwa jina la
Tausi Saidi (29), mkazi wa Mbete katika Manispaa ya Morogoro,
alifikishwa hospitalini hapo na muuguzi wa Zahanati ya Mbete iliyopo Kata ya Mlimani akiwa ameambatana na ndugu zake  Januari 7, saa 10 jioni akiwa anaumwa uchungu.

Hata hivyo mume wa mwanamke huyo, Kudra Khalfani alisema kwamba mke wake alianza kupata uchungu na hivyo kumpeleka Zahanati ya Mbete.

Baada ya kufika huko, alilazimika kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya kuonyesha dalili za kujifungua. Baada ya kufika wodi ya wazazi, nesi waliyeambatana naye aliyemtaja kwa jina moja la Mwacha, aliingia wodini na kumtaka kwenda kumwangalia mgonjwa wito ambao alidai haukuitikiwa na muuguzi huyo.

Mwanaume huyo alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida, muuguzi huyo aliwataka kumpeleka mama huyo wodi namba saba ‘B’ bila kutoa msaada wowote ikiwa ni pamoja na kujua hali ya mgonjwa.

Nionavyo kuhusu tukio hili, sekta zinazohusika na kitengo hiki zifanye uchunguzi juu ya tukio hili kwa undani zaidi ili  wahusika waliofanya kitendo hiki waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hili limefanyika katika hospitali ya rufaa ambayo ipo mjini huko vijijini hali ni mbaya zaidi kwakua hakuna viongozi wa karibu wanaoogopwa na wauguzi.

0713-804343-esthermacha10@gmail.com

No comments:

Post a Comment