07 January 2013
Wabunge Arusha watakiwa kuhudhuria vikao vya ALAT
Na Queen Lema,Longido
WABUNGE wa Mkoa wa Arusha wametakiwa kuhakikisha kuwa wanahudhuria kwenye Vikao vya Jumuiya za Serikali za Mitaa (ALAT) na kuachana na tabia ya kukwepa vikao hivyo kwani michango ya yao inaweza kuimarisha jumuiya hiyo pamoja na mkoa ambao unahitaji majibu badala ya maswali kutoka kwa viongozi.
Hayo yameelezwa jana wilayani Longidio na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa kwa Tawi la Arusha(ALAT),Goodson Majola katika kikao cha wadau wa jumuiya hiyo na viongozi wake.
Majola alisema kuwa wabunge wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanahudhuria vikao kwa kuwa wanajua na kutambua shida na changamoto mbalimbali ambazo zimo kwenye jamii lakini kama watakuwa hawahudhurii vikao bado jamii itaendelea kuwa na changamoto mbalimbali.
Aliongeza kuwa wabunge wanapokwepa vikao mbalimbali hasa vya jumuiya za Serikali za Mitaa kunasababisha maendeleo kuwa hafifu sana kwenye jamii huku wananchi nao wakiwa na hisia tofauti tofauti juu ya utendaji kazi wa wabunge hao pamoja na Halmashauri zao.
“Sasa hivi wabunge wanatakiwa kujua na kutambua kuwa jamii ambayo inaongoza haitaji maswali bali inahitaji majibu na hii pia ni hata ndani ya halmashauri zetu kwa hiyo mpaka sasa wabunge wanatakiwa kutumia jumuiya hii na kushirikiana na kisha kutatua kero za jamii,lakini kama watakuwa wanakimbia vikao ni wazi kuwa jumuiya hii haitaweza kufikia malengo yake, ”alisema Majola.
Katika hatua nyingine katibu wa jumuiya hiyo, Khalifa Idda alisema kuwa endapo kama wadau mbalimbali pamoja na watalamu wa Halmashauri za Mkoa wa Arusha wataweza kutumia jumuiya hiyo vema basi wataweza kusaidia hata halmashauri kuepukana na hati chafu ambazo zimekuwa zikisumbua sana baadhi ya halmashauri.
Idda alisema kuwa kupitia Jumuiya hiyo wataweza kujadili mambo mbalimbali ambayo yanasababisha kupata hati chafu hivyo suala kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) litakuwa ni ndoto hivyo kuongeza hata ufanisi zaidi wa kimapato.
“Suala la hati chafu limekuwa kikwazo kikubwa sana kwenye halmashauri zetu lakini kama watu watakuwa na umoja na watashiriki kwa undani sana kwenye ALAT basi wataepukana na hilo kwa kuwa hapa tutaweza kujadili kwa wale waliofanikiwa kuvuka, ”alisema Idda.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment